Sep 28, 2023 11:36 UTC
  • Mgogoro wa Afya ya Akili na Kujiua katika Jamii ya Marekani (Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani)

Jumapili ya tarehe 10 Septemba ilisadifiana na Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kujiua. Siku hiyo ilisajiliwa katika kalenda ya dunia mwaka wa 2003 na Chama cha Kimataifa cha Kuzuia Kujitoa Uhai kwa ushirikiano wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

 Madhumuni kuu ya kuanzishwa siku hiyo ni kuongeza ufahamu kuhusu vitendo vya kujiua kwa mashirika, serikali na umma kwa ujumla na kuzidisha umakini kwenye tatizo la afya ya akili ili kueleza kwamba, kujiua kunaweza kuzuiwa. Kwa sababu hiyo, kila mwaka Shirika la Afya Duniani (WHO) huainisha kauli mbiu kama ajenda kuu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa na jumuiya za kimataifa kwa ajili ya kuzuia vitendo vya kujitoa uhai. Kauli mbiu iliyoainishwa kwa ajili ya miaka mitatu ya kuanzia 2021-2023 ni: "Kujenga Tumaini Kupitia Matendo" (Creating Hope Through Action). Kauli mbiu hiyo inatoa wito wa kuchukua hatua za kivitendo na kukumbusha kwamba, kuna njia mbadala ya kujiua, na kwamba tunaweza kutia matumaini katika nyoyo za watu kupitia matendo yetu.

Ripoti ya iliyochapishwa Agosti 28, 2023 na Shirika la Afya Duniani (WHO) inaonyesha kuwa, zaidi ya watu 700,000 hujitoa uhai kila mwaka kote duniani. Takwimu hii inakuwa ya kutisha zaidi tunapojua kwamba, makadirio yanaonyesha kuwa watu milioni 14 hadi 15 hufanya jaribio la kujiua kila mwaka duniani, lakini ni karibu 700,000 tu kati yao wanaofanikiwa kujitoa uhai. Kulingana na takwimu hizo, majaribio ya kujiua miongoni mwa wanawake ni mara mbili ya wanaume, lakini majaribio yanayofanikiwa ya kujiua ya wanaume ni mara tatu hadi nne zaidi ya wanawake. Pia, kujiua ni sababu ya nne ya vifo kati ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 29 duniani, na husababisha asilimia 50 hadi 71 ya vifo vyote vya kikatili kwa wanaume na wanawake, kwa mpangilio.

Hii leo, kujiua limekuwa janga la kimataifa; na licha ya dhana potofu kwamba kujiua kunazihusu nchi masikini au zinazoendelea tu, na kwamba nchi tajiri duniani hazikabiliwi na tatizo hilo, lakini mapitio ya ripoti za hivi karibuni na data za takwimu za mashirika ya kimataifa zinaonyesha kuwa, kujiua hakuhusiani tu na nchi zenye kipato cha chini, bali hutokea duniani kote; na nchi nyingi zilizoendelea pia zina viwango vya juu zaidi vya takwimu za kujitoa uhai. Kwa mfano, kwa mujibu wa takwimu za 2021 za kiwango cha watu wanaojiua duniani, ingawa nchi maskini ya Afrika, "Lesotho", ilishika nafasi ya kwanza katika kiwango cha watu wanaojiua, mwaka huo huo, Korea Kusini, ambayo inatambuliwa kuwa moja ya nchi zilizoendelea na zinazoongoza kiuchumi duniani, ilishika nafasi ya nne; na katika 2019, Japan ilishika nafasi ya tano.

Idadi ya watu wanaojiua katika nchi ya Marekani imeongezeka sana katika miaka miwili mpaka mitatu iliyopita na vitendo hivyo vimeenea hata miongoni mwa watoto na barobaro. Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya Wamarekani 44,000 hufa kwa kujiua kila mwaka, na kujiua ni moja ya sababu 10 kuu za vifo nchini humo. Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya Wamarekani 44,000 hufa kwa kujiua kila mwaka, na kujitoa uhai ni moja ya sababu 10 kuu za vifo nchini humo. Takwimu zinasema, mwaka 2015, kujiua ilikuwa sababu ya 14 ya vifo vya wanawake, na sababu ya 7 ya vifo vya wanaume nchini Marekani. Zaidi ni kwamba, kujiua ni sababu ya pili ya vifo vya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 34, na sababu ya tatu ya vifo kwa watu wenye umri wa miaka 10 hadi 14. 

Kuanzia 1999 hadi 2010, kiwango cha kujiua kati ya Wamarekani wenye umri wa miaka 35 hadi 64 kiliongezeka kwa karibu asilimia 30. Ongezeko kubwa zaidi lilikuwa kati ya wanawake wenye umri wa miaka 60 hadi 64, ambako kiwango cha kujiua kiliongezeka kwa 60%; kisha vifo vya wanaume kutokana na kujiua wakiwa na umri wa miaka 50 viliongezeka kwa asilimia 50, suala ambalo linaonyesha mgogoro mkubwa wa kijamii huko Marekani.

Data za Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) zinaonyesha kuwa, kiwango cha kujiua kati ya Wamarekani mwaka jana kiliweka rekodi katika historia ya nchi hiyo. Kulingana na takwimu hizi, Wamarekani wasiopungua 49,449 walijiua mnamo 2022, kiwango ambacho ni takriban vifo 15 kwa kati ya kila watu laki moja. Kwa takwimu hii, kiwango cha kujiua katika jamii ya Marekani kiliipiku rekodi ya awali ya mwaka 2018 na kiliongezeka kwa 5% ikilinganishwa na mwaka 2018. Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, mnamo 2021, 25% ya vifo vya watoto wa miaka 10-17 nchini Marekani vilitokana na kujiua, ambayo ilikuwa sababu ya pili kuu ya vifo katika kundi hili la umri mwaka huo.

Idadi ya wanaojiua katika jeshi la Marekani pia ni ya kushangaza, na tangu mwanzoni mwa 2020 hadi mwisho wa Septemba 2021, idadi hiyo ilizidi ile ya wanajeshi wa Marekani ambao wameaga dunia kutokana na virusi vya corona tangu mwanzoni wa janga hilo. Ripoti zinaonyesha kuwa, mwaka 2020, wanajeshi 701 wa Marekani walijitoa uhai wenyewe, na idadi hii ilifikia wanajeshi 476 katika miezi tisa ya kwanza ya 2021. Hii ni licha ya kwamba, tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona nchini Marekani, wanajeshi 886 wa nchi hiyo tu wamefariki dunia kutokana na virusi hivyo. 

Kwa mujibu wa ripoti ya kushtua iliyotolewa katika majira ya joto ya mwaka huu 2023, wanajeshi 30,177 wa Marekani wakiwemo maveterani waliopigana katika vita vya nchi hiyo tangu mashambulizi ya 9/11 mwaka 2001 wamekufa kwa kujitoa uhai wao wenyewe. Hii ni licha ya kuwa jumla ya wanajeshi 7,057 wa Marekani wameuawa katika vita vyote ambavyo Wamarekani wameanzisha tangu mwaka huo.

Awali, ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani pia ilionyesha kuwa, kiwango cha kujiua kati ya wanajeshi wa nchi hiyo kiliongezeka kwa 41.4% kati ya 2015 na 2020.

Ni vyema pia kuashiria hapa kuwa, uchunguzi wa ripoti na takwimu mbalimbali za watu waliojiua katika jamii ya Marekani unaonyesha kuwa silaha za moto, yaani bunduki, zilichangia zaidi ya nusu ya vifo vya kujiua wenyewe nchini Marekani mwaka wa 2022. Ripoti iliyochapishwa Juni 2023 na Kituo cha Johns Hopkins pia inasisitiza kwamba, kwa ujumla, kujiua kwa bunduki kumekuwa sababu kuu ya ongezeko la hivi karibuni la kiwango cha kujitoa uhai huko Marekani. Ripoti hiyo inasema, kiwango cha watu wanaojiua kwa kutumia bunduki kiliongezeka kwa 10% kati ya 2019 na 2021, huku kiwango cha watu wanaojiua bila ya kutumia bunduki kikipungua kwa 8% katika muda huo huo. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa, wanaume wazungu, pamoja na watu wengine wenye umri wa miaka 75 na zaidi, ndio waliojiua zaidi kwa bunduki mwaka wa 2021.   

Kwa kuzingatia hayo yote, inaonekana kwamba jamii ya Marekani imekumbwa na mgogoro mkubwa ya afya ya akili. Ukweli huu unathibitishwa na kura ya maoni iliyofanywa mwaka jana (2022) na mtandao wa habari wa CNN kwa ushirikiano na Kaiser Family Foundation. Matokeo ya uchunguzi huo yanaonyesha kuwa, watu wazima 9 kati ya kila watu 10 nchini Marekani wanaamini kwamba, nchi yao inasumbuliwa na tatizo la afya ya akili. Katika uchunguzi huo, zaidi ya mtu 1 kati ya watu wazima 5 walisema kuwa afya yao ya akili ni duni na dhaifu, na theluthi moja ya watu wote wazima walisema, nyakati zote au mara nyingi walihisi hali ya wahka na mfadhaiko katika kipindi chote cha mwaka uliopita. Takriban 1 kati ya kila watu wazima 5 pia alisema, mara nyingi au daima alikuwa na sonona, mfadhaiko au kujihisi mpweke katika mwaka uliopita.

Data hizi zinaonyesha kuwa, afya ya akili imekuwa changamoto kubwa ya afya ya umma na ya kijamii katika jamii ya Marekani, na watu wengi na familia zao wanasumbuliwa na hali ya kujisikia upweke na kutokuwa na thamani. Vilevile inaonekana kuwa, tatizo la afya ya akili linalowasumbua Wamarekani halielekei kupungua, kwani takwimu za muda za mwaka jana 2022 zilionyesha kuwa, vitendo vya kujitoa uhai mwaka huo viliongezeka kwa asilimia 2.6 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.  

Tags