Nov 13, 2018 08:46 UTC
  • Adhama ya Maulidi (Kuzaliwa) ya Mtume Muhammad SAW

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum wasikilizaji wapenzi. Kama mnavyojua, tumo ndani ya Mfunguo Sita, mwezi ambao alizaliwa Bwana wetu Muhammad SAW. Leo katika dakika hizi chache, tutazungumzia adhama ya kuzaliwa mtukufu huyo tukiwa na matumaini mtakuwa nasi hadi mwisho wa maelezo haya mafupi.

Maulidi kwa maana ya kuzaliwa Mtume Mtukufu si tukio la kihistoria tu, bali ni tukio muhimu mno la kuainisha hatima ya mwanadamu. Matukio yaliyoambatana na maulidi hayo matakatifu kama ilivyoripotiwa katika historia yenyewe yalikuwa ni ishara ya wazi iliyobainisha maana halisi na uhakika wa mwana mtukufu aliyezaliwa, Muhammad al Mustafa SAW.

Imenukuliwa kwamba, katika zile sekunde za kuzaliwa Mtume Mtukufu (rehema za Allah ziwe juu yake na Aali zake) nembo za kufru na shirki zilikumbwa na zilizala na pigo kubwa katika sehemu mbalimbali duniani. Moto wa Fars (Uajemi) ambao ulikuwa unawaka kwa muda wa miaka elfu bila ya kuzimika, ulizimika siku hiyo ya kuzaliwa Mtume. Masanamu yaliyokuweko kwenye maabadi na masinagogi mbalimbali yalianguka na kuwafanya watawa na wahudumu wa masinagogi na maabadi hayo wachanganyikiwe na kushindwa kujua nini kimetokea! Matukio hayo yaliyosadifiana na lahdha ya kuzaliwa Mtume yalikuwa ishara ya kuporomoka misingi yote ya shirki na ukafiri.

Mtume Muhammad SAW alizaliwa huko Makka katika Bara Arabu. Baba yake ni Abdullah mwana wa Abdul Muttalib mwana wa Hashim. Mama yake ni Bi. Amina Bint Wahab. Babu yake Abdul Muttalib alikuwa na wake wengine watano, na Abdullah yaani baba yake mzazi Mtume pamoja na Abu Talib ami na mlezi wake Mtume SAW, walitoka katika tumbo moja. Mtume Muhammad SAW alizaliwa akiwa yatima, kwani baba yake yaani Abdullah bin Abdul Muttalib alifariki dunia miezi mitatu kabla ya kuzaliwa mtukufu huyo.

Katika upande mwingine kasri la wafalme majabari na washirikina wa wakati huo wa Iran lilikumbwa na mtetemeko mkubwa na mabaraza ya Kasri la Madain - yale mabaraza 14 - yaliporomoka. Hiyo ilikuwa ni ishara nyingine ya kimaanawi iliyothibitisha kuwa kulitokea jambo kubwa na lisilo la kawaida wakati huo na kwamba, maulidi na kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW ulikuwa ni utangulizi wa mazingira ya kupambana na ukafiri na mataghuti wa dunia nzima. Naam, maulidi na kuzaliwa mtukufu huyo wa daraja kumeleta mapinduzi makubwa mno katika upande wa umaanawi na uongofu wa moyo na fikra kwa mwanadamu na pia katika upande wa miongozo ya kijamii na kivitendo kwa ajili ya matabaka mbalimbali ya mwanaadamu. Kupambana na dhulma, kupiga vita utaghuti, kukabiliana vilivyo na utawala usio wa haki wa madhalimu wanaokandamiza watu, ni sehemu tu ya ishara nyingi za kimaanawi na adhama ya kuzaliwa Mtume.

Maulidi na kuzaliwa Bwana Mtume SAW kwa kila Muislamu ni nukta na jambo muhimu mno katika historia. Kwani kuzaliwa mtukufu huyo ndiko baadaye kulikopelekea kutokea harakati kubwa isiyo na kifani katika historia ya mwanadamu. Kila fadhila, neema na baraka zilizoko katika ulimwengu huu, chanzo chake ni kuzaliwa na kubaathiwa yaani kupewa Utume mbora huyo wa umbo na tabia na ndio maana kusimamishwa misingi ya tabia njema duniani, kunatokana na baraka za kuweko kwake mtukufu huyo. Kila Muislamu anatambua kwamba, hakuna nukta na jambo bora la kuukutanisha pamoja umma wa Kiislamu ghairi ya itikadi na imani yao kwa Mtume wa Uislamu. Wafuasi wa madhehebu mbalimbali huweka kando hitilafu zao ndogo ndogo na kuafikiana kutokana na baraka za kuweko Mtume wao mmoja. Waislamu wote wanampenda Mtume na yeye kwa hakika amekuwa mhimili na nguzo imara na madhubuti ya umma wa Kiislamu katika kipindi chote cha historia. Ni kwa kuzingatia hilo ndio maana tunasema kuwa, kuadhimisha maulidi na siku ya kuzaliwa Mtume SAW ni muhimu kwetu sisi sote. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags