Jan 20, 2021 02:40 UTC
  • Human Rights Watch yakosoa hali ya haki za binadamu nchini Morocco

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limekosoa hali ya haki za binadamu nchini Morocco na kutangaza kuwa, maafisa wa nchi hiyo wamezidisha mminyo na ukandamizaji wa uhuru wa raia.

Human Rights Watch imeeleza katika ripoti yake kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Morocco kwamba, baadhi ya watu waliokamatwa wamewekwa mahabusu kwenye vyumba vya mtu mmoja mmoja kwa muda wa siku 23 na kunyimwa fursa ya kuwasiliana na mahabusu wengine, ukiwa ni muamala mbaya na ukiukaji wa vigezo vya kimataifa.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa, maafisa wa Morocco wangali wanaendelea kukwamisha uundwaji wa asasi za kiraia na ufanyaji kazi wa asasi hizo.

Sehemu nyingine ya ripoti ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu imeeleza kuwa, kati ya Septemba 2019 hadi Januari 2020, mamlaka za Morocco ziliwakamata na kuwafungulia kesi watu kadhaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kwa sababu ya jumbe walizotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook au mikanda ya video waliyorusha kwenye mtandao wa YouTube.

Mfalme Muhammad VI wa Morocco

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, watu hao walishtakiwa kwa makosa ya kumvunjia heshima mfalme wa Morocco, kuchafua sura ya taasisi za utawala na kuwatusi wafanyakazi wa serikali.

Wanaharakati wa kiraia nchini Morocco wanasema, mageuzi na ahadi za mabadiliko katika utawala alizokuwa ametoa mfalme Muhammad VI wa nchi hiyo ni za kimaonyesho tu na hazijawa na tija yoyote ile.../ 

Tags