Jan 23, 2021 05:02 UTC
  • Kikao cha Baraza la Usalama kuhusu mapigano ya Darfur chamalizika bila ya natija

Kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoitishwa kujadili mapigano ya karibuni katika eneo la Darfur maagharibi mwa Sudan kimemalizika bila ya natija.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha faragha kufuatia ombi la nchi za Ulaya na Marekani ili kuyapatia ufumbuzi mapigano ya karibuni huko Darfur magharibi mwa Sudan hata hivyo kikao hicho kimeshindwa kutoa taarifa ya pamoja au kufikia mapatano juu ya namna ya kutatua hali ya mambo katika eneo hilo. 

Nchi za Ulaya, Marekani na Mexico zimependekeza katika kikao hicho  kuidhinisha taarifa kufuatia ombi la Sudan la kutaka kuharakishwa utekelezaji wa mipango yake ya kuwalinda raia, hata hivyo nchi za bara la Afrika wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na India, Russia, na China zimepinga ombi hilo na zimetaka kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala nchi ya Sudan.  

Wakati huo huo taarifa ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa, watu 200 wameuawa na wengine 240 wamejeruhiwa katika mapigano makali ya kikabila yaliyojiri hivi karibuni katika jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan. Vita kati ya serikali ya Sudan na makundi ya wanamgambo wenye silaha katika jimbo la Darfur vilianza tangu mwaka 2003; na hadi sasa mapigano hayo yamesababisha vifo vya watu laki tatu  na kusababisha wengine milioni mbili na laki tano kuwa wakimbizi. 

Jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan lililokumbwa na mapigano 

 

Tags