Apr 04, 2021 10:58 UTC
  • Raia 50 wa Afrika Kusini watoweka kufuatia shambulio la kigaidi Msumbiji

Afrika Kusini imesema raia wake zaidi ya 50 hawajulikani walipo mpaka sasa baada ya magaidi kuvamia na kuudhibiti mji wa Pwani wa Palma nchini Msumbiji, huku taarifa zikisema kuwa makumi ya watu wameuawa katika shambulio hilo.

Siphiwe Dlamini, Afisa Habari wa Wizara ya Ulinzi na Maveterani wa Kijeshi ya Afrika Kusini amesema, mbali na raia mmoja wa nchi hiyo kuthibitika kuwa ameuawa katika shambulio hilo, lakini wengine zaidi ya 50 wametoweka.

Hata hivyo amesema raia wengine 50 waliokuwa wameripotiwa kutoweka hapo awali kupitia ubalozi wa Afrika Kusini mjini Maputo wamepatikana, na mchakato wa kuwarejesha nyumbani kwa wale wanaotaka unaendelea. 

Dlamini ameongeza kuwa, Afrika Kusini itashiriki mkutano wa Troika ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliotishwa na Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi kujadili kadhia ya Msumbiji.

Wakazi karibu 80 elfu wa mji wa Palma wamekimbia makazi yao

Magaidi waliuvamia mji wa Palma katika mkoa wa Cabo Delgado mwishoni mwa mwezi uliopita wa Machi, katika tukio ambalo ni kubwa kutokea tangu watu wenye silaha kuanzisha mashambulizi kaskazini mwa Msumbiji mwaka 2017.

Jeshi la Msumbiji linaendeleza oparesheni kubwa ya kukomboa mji huo wa pwani unaodhibitiwa na kundi la kigaidi linalojiita al-Shabaab. Hivi karibuni, magaidi wa Daesh (ISIS) walitangaza kuwa wao ndio waliouteka mji huo wa Palma tarehe 24 Machi. 

Tags