Jul 20, 2021 07:42 UTC
  • Jihad Islami: Tutailinda al Aqsa kwa nguvu zote

Harakati ya Jihad Islami ya Palestina imetoa tamko kuhusu hujuma iliyofanywa na Wazayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al Aqsa katika Siku ya Arafa na kutangaza kuwa, vita vya Panga la Quds bado havijaisha na taifa la Palestina liko tayari kulinda eneo hilo takatifu.

Taarifa iliyotolewa na Jihadi Islami usiku wa kuamkia leo imesema kuwa, hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuwaruhusu walowezi kuingia katika Msikiti wa al Aqsa katika siku hizi tukufu za mazingira ya Siku ya Arafa na kumi la kwanza la Mfunguo Tatu Dhulhija ni uchokozi dhidi ya Waislamu na kukanyaga hisia za wafuasi wote wa dini hiyo. 

Imesema lengo la siasa hizo za kihasama ni kutaka kuzusha machafuko na kwamba mradi huo hatari wa ukoloni wa Wazayuni hauwezi kusimamishwa isipokuwa kwa kutumia mabavu.

Jumatatu ya jana sambamba na maadhimisho ya Siku ya Arafa huko Palestina, makumi ya walowezi wa Kizayuni waliokuwa wakipewa himaya na ulinzi wa polisi ya Israel walivamia tena viwanja vya Msikiti wa al Aqsa na kuwashambulia Wapalestina waliokuwa ndani ya msikiti huo. 

Askari wa Israel pia waliwalazimisha Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ndani ya Msikiti wa al Aqsa kuondoka eneo hilo na kuwaruhusu walowezi wa Kizayuni kuvamia msikiti huo. 

Tags