Jul 27, 2023 10:20 UTC
  • Afrika Kusini: Baraza la Usalama la UN limeifelisha dunia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesisitizia udharura wa kufanyiwa mabadiliko muundo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa akisisitiza kuwa, chombo hicho kimeifelisha dunia kwa kutofanya kazi inavyotakiwa.

Naledi Pandor amesema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na televisheni ya Russia Today, kabla ya kuanza mkutano wa kilele wa Russia na Afrika ulioandaliwa huko Saint Petersburg kati ya leo na kesho Julai 28.

Amesema kuwa, "Tunapozungumzia mageuzi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, tunakusudia uwakilishi mpana zaidi na michakato (komavu) ya demokrasia. Baraza la Usalama limeifelisha dunia kwa kuwa limeshindwa kuzuia migogoro mingi inayoshuhudiwa kote duniani hivi sasa."

Pandor amesema Afrika Kusini inaunga mkono wito wa kutolewa kiti cha kudumu cha Baraza la Usalama kwa bara la Afrika na kuongeza kuwa, Baraza la Usalama linapaswa kuwa na wawakilishi kutoka nchi za Asia, Afrika na Amerika Kusini.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Afrika Kusini amebainisha kuwa, umewadia wakati wa kulifanyia marekebisho Baraza la Usalama pamoja na mfumo wa ubadilishaji wa fedha ulimwenguni ili viendanane na hali ya duni ya sasa.

Baraza la Usalama la UN

Pandor ameashiria kuendelea kuimarika kundi la BRICS linaloongozwa na mataifa yanayoinukia kiuchumi duniani ya Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini na kueleza kuwa, BRICS inafanya juhudi za kujaza pengo lililosababishwa na mapungufu ya Baraza la Usalama, katika kudhamini usalama na amani kote duniani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ameongeza kuwa, "Sisi (BRICS) hatusimami dhidi ya yeyote au kumtetea yeyote, lakini tunafanya kazi kwa maslahi ya dunia. BRICS inapinga kugeuzwa silaha kitu chochote kile." 

 

Tags