Aug 21, 2023 10:17 UTC
  • Misri yamkamata mwandishi habari aliyefichua utambulisho wa maafisa waliokuwa kwenye ndege iliyokamatwa Zambia

Mtandao wa Middle East Eye umeripoti kuwa askari usalama wa Misri wamemkamata mwandishi wa habari Karim Al-Asaad, kwa sababu ya kuchapisha makala kwenye vyombo vya habari kuhusu maafisa wa serikali ya Cairo waliokuwa kwenye ndege ya kibinafsi, ambayo ilikamatwa na mamlaka ya Zambia katika wiki iliyopita.

Mke wa mwandishi habari Karim Al-Asaad amesema kwamba, mumewe amekamatwa akiwa kwenye nyumba ya familia yake katika kitongoji cha Al-Shorouk mjini Cairo baada ya nyumba hiyo kuvamiwa na askari usalama na kutishia maisha ya mtoto wao.

Karim Al-Asaad

Ripoti zinasema, ndege hiyo ilikuwa imesheheni mamilioni ya pesa taslimu dola za Marekani, pamoja na kiasi kikubwa cha dhahabu, na baadhi ya silaha. Taarifa hizo zinasema kuwa meja wa jeshi la Misri alikuwa ndani ya ndege hiyo pamoja na maafisa wengine kadhaa wa serikali ya Cairo.

Mamlaka ya Zambia ilipata zaidi ya dola milioni 5.7 fedha taslimu, kiwango kikubwa cha dhahabu na bunduki tano zenye risasi 126.

Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema ameonya kuwa watu wote waliohusika katika sakata ya dhahabu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenneth Kaunda watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Zambia, Lusaka siku ya Ijumaa iliyopita, Hichilema alisema kuwa uhalifu huu utapigwa vita bila kujali nafasi na vyeo vya watu waliohusika.

Amesema kuwa nchi yake iko wazi kwa biashara na uwekezaji, akisisitiza kuwa "hakuna nafasi ya vitendo vya uhalifu nchini Zambia."

Tags