Afrika Kusini yavunja uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel
Kufuatia kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa la Palestina, wabunge wa Afrika Kusini wamepiga kura ya kufunga ubalozi wa utawala wa Kizayuni nchini humo. Kwa uamuzi huo, ubalozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Afrika Kusini utafungwa, uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo utakatwa na balozi wa utawala huo wa Kizayuni kutimuliwa kutoka Pretoria.
Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi kubwa na zenye ushawishi mkubwa katika bara la Afrika ambayo baada ya kupitia uzoefu mgumu wa ubaguzi wa rangi; sasa inaongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na tawala za ubaguzi wa rangi ulimwenguni kote.
Watu wa nchi hiyo, ambao walipambana kwa miongo kadhaa chini ya uongozi wa Nelson Mandela dhidi ya ubaguzi wa rangi wa serikali iliyoongozwa na wazungu waliowachache, hatimaye waliweza kupata ushindi. Kwa miaka sasa, taifa la Afrika Kusini kwa ushirikiano na serikali limekuwa mstari wa mbele kupiga vita ubaguzi wa rangi duniani.
Kwa mujibu wa viongozi wa Afrika Kusini, utawala wa Israel ni utawala wa ubaguzi wa rangi au apathaidi unaowachukulia Mayahudi kuwa watu bora kuliko Waislamu wa Palestina na kwa msingi huo unawabagua.
Kwa hiyo, katika miaka ya hivi karibuni, Afrika Kusini daima imechukua msimamo dhidi ya ubaguzi wa rangi wa Israel katika ardhi ya Wapalestina. "Naledi Pandor", Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini, anasema katika muktadha huu kwamba: "Kadhia ya Palestina inatukumbusha historia ya Afrika Kusini ya ubaguzi wa rangi na ukandamizaji. Kama Waafrika Kusini, tumejionea wenyewe athari za kukosekana usawa wa rangi na ubaguzi, na hatuwezi kukaa bila kufanya lolote huku kizazi kingine cha Wapalestina kikiwa kinabaguliwa na kuwekwa katika nafasi ya chini katika jamii."
Kuhusiana na hilo, tangu kuanza vita vya Gaza na kushadidi mauaji ya Wapalestina yanayofanywa na Israel, mara kadhaa serikali ya Afrika Kusini imekuwa ikitoa kauli dhidi ya ukandamizaji wa Israel na kutoa wito wa kukomeshwa vita huko Gaza. Hata hivyo kutokana na muendelezo wa jinai za Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, Afrika Kusini imevitaja vitendo hivyo kuwa ni uhalifu wa kivita, ambapo Naledi Pandour, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema: "Mauaji ya kimbari hayawezi kuvumiliwa mbele ya macho ya jamii ya kimataifa, na serikali ya Afrika Kusini imeamua kuwaita nyumbani wanadiplomasia wetu kutoka Tel Aviv."
Kadhalika, kutokana na kuendelea vita vya maangamizi ya umati vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, viongozi wa Afrika Kusini wamewasilisha rasmi malalamiko dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Pretoria pia imeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kumkamata Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwa tuhuma za mauaji ya halaiki.
Sasa, baada ya kauli hizi, Afrika Kusini imeamua kuvunja uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia na utawala haramu wa Israel.
Kwa mtazamo wa wananchi na viongozi wa Afrika Kusini, kuwaunga mkono watu wa Palestina ni suala muhimu na la kimsingi ambalo linahitaji hatua za kivitendo. Wananchi wa Afrika Kusini wanaamini kuwa watu wa Palestina wana haki ya kudai kujitawala, kutawala nchi yao huru, na kuishi kwa uhuru na bila kubaguliwa.
Nkosi Zwelivelile Mandela, mjukuu wa Nelson Mandela na mmoja wa watetezi wa kadhia ya Palestina, anasema kuhusiana na maudhui hii kwamba: "Wapalestina wanahitaji kuungwa mkono kivitendo kwa ajili ya uhuru."
Kwa vyovyote vile, hatua ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel inajiri wakati utawala huo wa Kizayuni umejitahidi sana kuboresha na kupanua uhusiano wake na nchi za Kiafrika katika miaka ya hivi karibuni kufuatia kufeli sera zake katika eneo la Asia Magharibi.
Hayo yanajiri wakati ambao nchi za Kiafrika, ambazo nyingi zimekumbwa na mzigo wa ubaguzi na ukandamizaji, sasa zimechukua msimamo dhidi ya Israeli na sera zake za unyakuzi wa ardhi za Palestina.
Hatua ya Afrika Kusini kuvunja uhusiano na utawala wa kibaguzi wa Israel, kwa kuzingatia nafasi na hadhi ya nchi hiyo katika bara la Afrika na dunia nzima, inaweza kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine kwa ajili ya kuonyesha kuwa dunia inapinga mauaji ya kimbari na jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina.