Wanajeshi wa Uganda watuhumiwa kutumia mabavu dhidi ya raia CAR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10702-wanajeshi_wa_uganda_watuhumiwa_kutumia_mabavu_dhidi_ya_raia_car
Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amewatuhumu wanajeshi wa Uganda walioko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwamba, wamekuwa wakitumia mabavu dhidi ya raia wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2016 09:34 UTC
  • Wanajeshi wa Uganda watuhumiwa kutumia mabavu dhidi ya raia CAR

Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amewatuhumu wanajeshi wa Uganda walioko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwamba, wamekuwa wakitumia mabavu dhidi ya raia wa nchi hiyo.

Cecile Pouilly, Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa amebainisha kwamba, wanajeshi wa Uganda walioko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa ajili ya kupambana na wanamgambo wa Kikristo wa kaskazini mwa Uganda wa LRA wamekuwa wakiwapora raia na kutumia mabavu dhidi yao. Aidha ripoti nyingine kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati zinaonesha kuwa, askari wa Uganda wamekuwa wakijihusisha pia na vitendo vya ubakaji.

Hayo yanajiri siku chache tu baada ya Zeid Raad al-Hussein, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa kutoa taarifa inayotahadharisha juu ya hatari ya kukaririwa tena machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Matukio ya hivi karibuni katika mji mkuu Bangui na katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo yamepelekea kuibuka wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa kusambaa haraka machafuko katika maeneo mengine ya nchi hiyo.