Mar 20, 2024 02:36 UTC
  • Hatua ya serikali ya Niger ya kufuta makubaliano ya kijeshi na Marekani

Amadou Abdurrahman, Msemaji wa Serikali ya Niger, ametangaza kupitia taarifa kwamba nchi hiyo imefuta makubaliano yote ya kijeshi na Marekani ambayo yaliruhusu nchi hiyo ya Magharibi kuweka majeshi yake katika ardhi ya Niger.

Msemaji huyo amesema: 'Serikali ya Niger, kwa kuzingatia matakwa na maslahi ya wananchi na sambamba na kutekeleza majukumu yake, imeamua kufuta makubaliano kuhusu kuwepo wanajeshi wa Marekani na wafanyakazi wa kiraia wa Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo katika ardhi ya Niger.'

Akisisitiza kuwa uwepo wa jeshi la Marekani ni kinyume cha sheria na unakiuka sheria zote za kikatiba na kidemokrasia, Abdurrahman amesisitiza kwamba makubaliano yaliyofutwa hayakuwa ya haki na kwamba yaliwekwa kwa maslahi ya upande mmoja na Marekani mnamo Julai 6, 2012.

Amadou Abdurrahman, Msemaji wa Serikali ya Niger

Marekani ilikuwa imetuma takriban wanajeshi elfu moja nchini Niger kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi. Mwishoni mwa mwaka jana (2023), serikali ya Niger pia ilifuta makubaliano ya ushirikiano wa kijeshi na Ufaransa na kuilazimisha nchi hiyo kuondoa vikosi vyake kutoka Niger mnamo Desemba 22.

Katika miaka ya hivi karibuni, nchi huru, zikiwemo nchi nyingi za Kiafrika, zimebadili mtazamo wao wa kisiasa katika uhusiano na ulimwengu wa nje na zinajaribu kupunguza utegemezi wao kwa Marekani na serikali za Magharibi katika maamuzi yao.

Viongozi wa baadhi ya nchi za Kiafrika wanajaribu kupunguza kiwango cha uhusiano wao na nchi hizo ili kupunguza uingiliaji wa kigeni na mivutano inayoibuliwa na serikali za Magharibi. Serikali za Ulaya zina historia ndefu ya kutawala na kuingilia masuala ya ndani ya nchi za Kiafrika, ambapo mwenendo wa serikali mbalimbali za Marekani katika miaka ya hivi karibuni pia umekuwa na lengo la kuingilia na kupora rasilimali za bara la Afrika.

Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, bara la Afrika lina rasilimali nyingi za chini ya ardhi ambazo ni muhimu sana kwa mashirika ya Magharibi. Afrika ina asilimia 96 ya almasi, asilimia 90 ya chrome, asilimia 85 ya platinam na karibu asilimia 30 ya thorium na urani inayopatikana kote duniani. Niger inachangia karibu asilimia tano ya urani inayouzwa ulimwenguni.

Urani ni madini ya mionzi ambayo hudhamini nishati ya nyuklia. Kulingana na Euratom, wakala wa nyuklia wa Umoja wa Ulaya, Niger ni muuzaji mkubwa wa pili wa urani asilia kwa umoja huo, ambapo hudhamini takriban asilimia 15 ya urani kwa Ufaransa.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali za Marekani na Ulaya zimekuwa zikiingilia masuala ya ndani ya nchi za bara hilo, zikiwemo Nigeria, Ivory Coast, Mali, Niger na Somalia kwa lengo la kupora rasilimali muhimu za madini za Afrika ambapo matokeo yake yamekuwa ni kuibuliwa migogoro ya kisiasa na kibinadamu barani humo.

Sehemu kubwa ya mivutano ya ndani katika nchi za Kiafrika pia inatokana na siasa kongwe za kikoloni za serikali za Ulaya. Hatua ya serikali ya Niger inaweza kutathminiwa kuwa ni juhudi za kurejesha uhuru wake na kujiepusha kuzitegemea nchi za Magharibi, na wakati huo huo ni onyo kwa Marekani na Ulaya kwamba bara la Afrika sio tena mtumwa na kibaraka wao kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Image Caption

Serikali za Kiafrika hazina tena hamu ya kuendelea kuzitegemea nchi za Magharibi kutokana na matokeo machungu ya uingiliaji wa Marekani na Magharibi katika masuala ya ndani ya bara la Afrika. Uwepo wa China na Russia katika bara hilo pia umekaribishwa na nchi wenyeji katika miaka ya karibuni, ambapo sasa serikali huru katika bara hilo zinakaribisha upanuzi wa uhusiano na Moscow na Beijing kutokana na uwezo wa nchi hizi mbili katika sekta ya uchumi.

Mwisho wa uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Niger unaonyesha kuwa, serikali za Afrika zimeamua kutafuta njia mbadala na kutozitegemea sana nchi za Magharibi katika kuimarisha usalama na uchumi wa nchi zao.

Tags