Judith Suminwa Tuluka ateuliwa kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kongo DR
(last modified Tue, 02 Apr 2024 06:15:11 GMT )
Apr 02, 2024 06:15 UTC
  • Judith Suminwa Tuluka ateuliwa kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke nchini Kongo DR

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amemteua waziri wa mipango Judith Suminwa kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo.

Suminwa ni mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa huo wa uwaziri mkuu nchini Kongo DR. Uteuzi wa Suminwa unakamilisha wiki kadhaa  zilizogubikwa na hali ya sutafahamu kuhusu wadhifa huo.

Katika hotuba aliyotoa kupitia televisheni ya taifa, Suminwa amesema, anafahamu kuhusu jukumu kubwa linalomkabili na akaongeza kuwa atafanya kazi kuhakikisha kunakuwepo amani na maendeleo nchini humo.

"Ninaelewa wajibu mkubwa nilionao... Tutafanya kazi kwa ajili ya amani na maendeleo ya nchi," alisema Bi Suminwa katika hotuba yake hiyo aliyotoa hapo jana.

Waziri Mkuu huyo mpya wa DRC ambaye ni Mchumi kitaaluma, anachukua nafasi ya uwaziri mkuu kutoka kwa Jean-Michel Sama Lukonde, kufuatia kuchaguliwa tena Tshisekedi kuwa rais mnamo Desemba 20.

Kuapishwa Tshisekedi kwa muhula wa pili madarakani mnamo mwezi Januari, kulianzisha mchakato wa muda mrefu wa kutafuta muungano wa vyama vingi katika bunge la taifa, hatua muhimu kabla ya kuteuliwa waziri mkuu na kuundwa serikali.

Rais Felix Tshisekedi na Waziri Mkuu mpya Judith Suminwa Tuluka

Suminwa atakuwa na jukumu la kutoa msukumo kwa vipaumbele vilivyotangazwa na rais Tshisekedi vya ajira, vijana, wanawake na uwiano wa kitaifa kwa taifa hilo lenye watu wapatao milioni 100.

Tshisekedi alishinda rasmi kwa asilimia 73.47 ya kura katika uchaguzi huo wa mwezi Desemba, ambao ulipita kwa amani kwa kiasi kikubwa katika nchi iliyokumbwa na ghasia na ukosefu wa utulivu kwa muda mrefu.

Hata hivyo Upinzani uliuelezea uchaguzi huo kuwa ni wa bandia.

Kiongozi huyo aliingia madarakani kuwa rais wa Kongo DR kwa mara ya kwanza mwaka 2019 akiahidi kuboresha hali ya maisha -katika nchi hiyo inayojivunia utajiri wa madini lakini ina idadi kubwa ya watu masikini - na kukomesha miaka 25 ya umwagaji damu katika eneo la mashariki.../

 

 

 

 

Tags