Mahakama Kuu Kenya yasimamisha uamuzi wa Bunge wa kumuidhinisha Kindiki kuwa Naibu Rais
(last modified Fri, 18 Oct 2024 13:53:32 GMT )
Oct 18, 2024 13:53 UTC
  • Mahakama Kuu Kenya yasimamisha uamuzi wa Bunge wa kumuidhinisha Kindiki kuwa Naibu Rais

Mahakama Kuu nchini Kenya leo imetoa amri ya muda ya kusimamisha kubadilishwa kwa Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ya Kenya umetangazwa dakika chache baada ya Bunge na Seneti kuidhinisha uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani, Kithure Kindiki, kama Naibu mpya wa Rais wa nchi hiyo.

Bunge la Kitaifa la Kenya leo Ijumaa lilikuwa limeidhinisha uamuzi wa Rais wa nchi hiyo, William Ruto, wa kumteua Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais baada ya kuondolewa madarakani aliyekuwa akishikiliwa wadhifa huo, Rigathi Gachagua.

Baada ya hapo, mawakili wa naibu rais aliyetimuliwa wamewasilisha ombi mahakamani kuzuia kuondolewa kwake afisini wakisema kuwa madai yaliyowasilishwa dhidi yake hayana msingi na hayaungwi mkono na ushahidi.

Sasa kesi hiyo itawasilishwa tena mahakamani tarehe 24 Oktoba, ambayo itatoa uamuzi kuhusu uhalali wa masuala ya kikatiba aliyoibuliwa.

Awali, wabunge 236 walipiga kura ya kuidhinisha uteuzi wa Rais William Ruto bila upinzani wowote. Wabunge wamelazimika kupiga kura mara mbili baada ya hitilafu ndogo ya kiufundi kutokea katika raundi ya kwanza kwa njia ya kielektroniki.

Spika Moses Wetangula amesema mapema leo kuwa Bunge limepasisha uteuzi wa Kindiki na kwamba Spika atawasilisha matokeo hayo kwa Rais. 

Bunge la KItaifa lamuidhinisha Profesa Kindiki 

Jana Alhamisi Maseneta wa Kenya wamempata Rigathi Gachagua na hatia ya makosa matano kati ya 11 yaliyowasilishwa dhidi yake yakiwemo ya ufisadi, kueneza siasa za chuki na ukabila.  

Kwa mujibu wa cheti chake cha kuzaliwa, Naibu Mpya Rais wa Kenya anafahamika kama Abraham Kithure Kindiki. Ni raia wa Kenya, aliyezaliwa Julai 16, 1972 katika Kaunti ya Tharaka Nithi. Profesa Kindiki amebobea katika masuala ya sheria na ana uzoefu pia katika masuala ya uongozi na utawala wa umma. 

Gachagua, ambaye amekanusha madai hayo, alipaswa kujitetea dhidi ya mashtaka katika Seneti Alhamisi alasiri kabla ya upigaji kura. Alipokosa kufika, wakili wake Paul Muite alisema naibu huyo wa rais alikuwa amelazwa hospitalini akiwa na maumivu makali ya kifua, na kuitaka Seneti kusitisha shughuli kwa siku kadhaa.

Tags