Morocco yaelekea Afrika Mashariki kutafuta uungaji mkono AU
Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco ameanza ziara ya nchi tatu za Afrika Mashariki katika juhudi za kutafuta uungaji mkono wa kurejea nchi hiyo kuwa mwananchama wa Umoja wa Afrika, baada ya kujiondoa kwenye umoja huo zaidi ya miongo mitatu iliyopita.
Akiwa mjini Kigali hapo jana, mfamle huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Paul Kagame wa Rwanda na wawili hao wakasaini hati 19 za maelewano, zinazonuia kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbali mbali. Haijabainika ni lini mfamle huyo ataondoka Rwanda kuelekea Tanzania, katika mkondo wa pili wa safari yake Afrika Mashariki na kisha kumalizia Ethiopia.
Mjumbe wa ngazi za juu ambaye ameandamana na mfamle huyo wa Morocco ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, ni masikitiko makubwa kuwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika haijawahi kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi za Afrika Mashariki, wala ushirikiano katika nyuga za uchumi, utamaduni na historia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco, Salahuddine Mezouar hivi karibuni amekuwa katika safari za kidiplomasia katika nchi kadhaa za Kiafrika zikiwemo Misri, Libya, Sudan, Senegal, Tunisia, Cameroon, Kodivaa na Ethiopia ili kuzitaarifu nchi hizo kuhusu uamuzi huo wa Rabat.
Ikumbukwe kuwa, Morocco iliamua kujiondoa katika Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) mwaka 1984 kufuatia uamuzi wa umoja huo wa kuafiki uanachama wa Jamhuri ya Sahara Magharibi iliyojitangaza kuwa huru. Morocco inaihesabu jamhuri hiyo kuwa ni sehemu ya ardhi yake.