Mashia Nigeria: Serikali inapanga kutuhujumu wakati wa Arubaini ya Imam Hussein AS
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema vyombo vya usalama nchini humo vinapanga kuwashambulia Waislamu wa madhehebu ya Shia wakati wa Arubaini ya Imam Hussein AS.
Msemaji wa harakati hiyo Ibrahim Musa, amesema wamepokea taarifa kuwa, maafisa wa kiintelijensia wa jeshi la nchi hiyo wanapanga kuzima maandamano ya amani ya kuadhimisha Arubaini ya Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume SAW, yaliyopangwa kufanyika Novemba 20.
Wakati huo huo, Kamisheni ya Haki za Bianadamu za Waislamu yenye makao makuu yake mjini London nchini Uingereza imempigia simu Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria kuhusu kadhia hiyo na kuitaka serikali yake iwadhaminie usalama Waislamu hao wa Kishia wataoshiriki maandamano hayo ya amani.
Mwezi uliopita, harakati hiyo ya Kiislamu ilipigwa marufuku katika jimbo la Kaduna, hatua ambayo ililalamikiwa vikali na watetezi wa haki za binadamu na makundi ya kiraia.
Siku chache zilizopita, Abdul Giwa, msemaji wa Harakati ya Kiislamu Nigeria alisema vyombo vya dola vimeanzisha 'kampeni ya umwagaji damu na uharibifu' dhidi ya Mashia wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, na kwamba harakati hizo zimechochewa na idiolojia ya Uwahabi ambayo chimbuko lake ni Saudi Arabia.
Mienendo hiyo ya kionevu ya serikali ya Abuja dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia imekuwa ikishuhudiwa tangu mwezi Disemba mwaka uliopita wa 2015, wakati askari wa jeshi la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika walipovamia mkusanyiko wa Waislamu katika mji wa Zaria, wakaua na kujeruhi maelfu ya watu mbali na kumtia nguvuni Sheikh Ibrahim Zakzaky.