Al Azhar: Uislamu umempa heshima kubwa mwanamke
(last modified Wed, 16 Nov 2016 07:55:03 GMT )
Nov 16, 2016 07:55 UTC
  • Sheikh Ahmad al Tayyib, Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri
    Sheikh Ahmad al Tayyib, Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri

Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri amesema kuwa, dini tukufu ya Kiislamu imempa heshima kubwa sana mwanamke na kutukuza nafasi yake muhimu katika jamii.

Shirika la habari la RASA limemnukuu Sheikh Ahmad al Tayyib akisema hayo wakati alipoonana na maafisa wa Baraza Kuu la wanawake Waislamu na wakuu wa makabila ya Nigeria na kusisitiza kuwa, dini tukufu ya Kiislamu imempa hadhi kubwa mwanamke na kuondoa dhulma yote aliyokuwa akifanyiwa kwa kumuweka daraja sawa na mwanamme katika masuala ya haki na ya kisheria.

Sheikh Ahmad al Tayyib pia amesema, vitendo vya kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) ni kinyume kabisa na mafundisho ya Uislamu na kubainisha kwamba, misimamo mikali, ukufurishaji na ukatili unaofanywa na magenge ya kigaidi kwa jina la Uislamu, ni vitu vilivyowaathiri pia wanawake suala ambalo ni kinyume kabisa na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Wanawake Waislamu nchini Nigeria

 

Mkuu huyo wa Chuo Kikuu cha al Azhar cha Misri amesema, wanawake wa Nigeria wana wajibu wa kusimama imara kukabiliana na genge la kigaidi na la wakufurishaji la Boko Haram ambalo linachafua sura ya Uislamu.

Kwa upande wao, wajumbe wa Baraza Kuu la Wanawake Waislamu wa Nigeria wamemshukuru Sheikhul Azhar kwa juhudi zake kubwa za kusimama imara kukabiliana na makundi ya kigaidi na kuonyesha sura sahihi ya dini tukufu ya Kiislamu.

Tags