Mgomo wa madaktari Kenya waingia siku ya 3, 20 waaga dunia
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mgomo wa madaktari na wauguzi katika hospitali za umma nchini Kenya imeongezeka na kufikia watu 20.
Watu 7 zaidi walifariki dunia hapo jana katika kaunti za Mombasa, Kisumu na Busia, katika siku ya pili ya mgomo huo. Tangu Jumatatu, madaktari wanaofanya kazi katika hospitali za serikali walianza mgomo wa nchi nzima, wakitaka kutimizwa makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2013 kati ya muungano wao na serikali kuhusu kuongezwa mishahara na kuboreshwa mazingira ya kufanyia kazi.
Hapo jana Waziri wa Afya wa Kenya Cleopa Mailu alisema mazungumzo kati ya serikali na wakuu wa miungano ya madaktari nchini humo yanaendelea, ingawaje hakuna matumaini ya kupatikana muafaka.
Hii ni katika hali ambayo, makumi ya wagonjwa wa akili waliotoroka katika Hospitali ya Mathari jijini Nairobi kufuatia mgomo huo wa madaktari hawajulikani walipo kufikia sasa.
Muungano wa Madaktari na Wauguzi Kenya ambao una wanachama wapatao elfu tano umeeleza kuwa, makubaliano hayo ya malipo yalipasa kuwapatia nyongeza ya mshahara ya asilimia 300, kujadili mazingira yao ya utendaji kazi na mifumo ya kazi, kuangalia upya vigezo vya kupandishwa cheo na kutatua tatizo la uhaba wa wafanyakazi wa huduma za afya mahospitalini.
Viongozi wa upinzani nchini humo wamekosoa kimya cha Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto juu ya mgogoro huo katika sekta ya afya, unaotishia maisha ya wengi.