HRW yataka Nigeria imuachie huru Zakzaky na iache kukandamiza Mashia
(last modified Thu, 15 Dec 2016 13:58:18 GMT )
Dec 15, 2016 13:58 UTC
  • HRW yataka Nigeria imuachie huru Zakzaky na iache kukandamiza Mashia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Abuja iheshimu agizo la mahakama na kumuachia huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigiera, Sheikh Ibrahim Zakzaky sambamba na kusitisha ukandamizaji dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo.

Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na Human Rights Watch imesema kuwa, vyombo vya dola nchini Nigeria vinafaa kumuachia huru mara moja Sheikh Ibarim Zakzaky na mkewe Zeenat ambao wamezuiliwa chini ya mazingira magumu kwa muda wa mwaka mmoja; kama ilivyoamuru mahakama moja nchini humo.

Hivi karibuni Jaji Gabriel Kolawole wa kitengo cha Abuja cha Mahakama Kuu ya Nigeria aliiamuru serikali imwachilie huru bila ya masharti yoyote Sheikh Zakzaky na mke wake katika kipindi cha siku 45 baada ya kutolewa agizo hilo.

Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakiandama kila uchao kushinikiza kuachiwa huru Zakzaky

Katika uamuzi wake huo Jaji Kolawole aliongeza kuwa kutokana na kukiuka haki za Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe na kutokana na wawili hao kushikiliwa kinyume cha sheria, kitengo cha huduma za usalama cha serikali kina wajibu wa kuwalipa kila mmoja fidia ya dola 79,000.

Hata hivyo, viongozi wa jimbo la Kaduna wangali wanashikilia kiongozi huyo wa kidini ashtakiwe na kuhukumiwa kifungo jela. Maafisa wa serikali ya jimbo la Kaduna walitangaza kuwa lazima Sheikh Ibrahim Zakzaky apandishwe kizimbani kwa kile walichodai "utovu wa sheria" uliofanywa na wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kwa muda wa miongo mitatu sasa. 

Sheikh Zakzaky baada ya kushambuliwa na wanajeshi wa Nigeria Disemba 2015

Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, Disemba 13 mwaka jana jeshi la Nigeria lilifanya hujuma dhidi ya Husseiniyah ya Baqiyatullah na makazi ya Sheikh Zakzaky mjini Zaria. Waislamu wapatao elfu moja waliuawa kwa umati na jeshi hilo likamtia mbaroni Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe.