Wafanyakazi 5 wa UN wauawa mpakani mwa Cameroon-Nigeria
Wafanyakazi watano wa Umoja wa Mataifa wameuawa katika mazingira ya kutatanisha na watu wasiojulikana katika mpaka wa Cameroon na Nigeria.
Taarifa iliyotolewa jana Jumatano na UN imesema kuwa, wafanyakazi hao wa umoja huo waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa Jumanne, baada ya wavamizi kuwashambulia walipokuwa wakiendelea na shughuli zao katika mji wa Kontcha, mpakani mwa nchi mbili hizo jirani.
Mohamed Ibn Chambas, Mwakilishi wa Maaulumu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Afrika Magharibi na eneo la Sahel amelaani hujuma hiyo na kusema kuwa, wafanyakazi hao wa UN waliouawa ni raia watatu wa Nigeria na wawili wa Cameroon.
Amefafanua kuwa, timu hiyo ya UN ilikuwa inaendesha shughuli ya kuanisha mpaka wa kilomita elfu 2 kati ya Cameroon na Nigeria, ambao umekuwa chimbuko la uhasama kati ya nchi mbili hizo jirani za magharibi mwa Afrika.
Umoja wa Mataifa umeripoti kuwa, Cameroon ni nchi ya pili baada ya Nigeria kukabiliwa na hujuma na mashambulizi ya magaidi wa kitakfiri wa Boko Haram.
Mwezi uliopita, Issa Tchiroma Bakary Waziri wa Mawasiliano wa Cameroon alitangaza kuwa wanajeshi na raia wa kawaida wa Cameroon zaidi ya 1500 wameuawa katika mashambulizi ya kundi la Boko Haram katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.