Mar 04, 2017 07:42 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika miripuko Maiduguri, Nigeria

Polisi nchini Nigeria imesema watu kadhaa waliuawa katika wimbi la mashambulizi ya mabomu katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo jana Ijumaa.

Victor Isuku, Mkuu wa Kamandi Kuu ya Polisi katika jimbo la Borno bila kutoa idadi kamili amesema watu kadhaa wameuawa katika milipuko hiyo ya mabomu iliyouitikisa mji wa Maiduguri, makao makuu ya jimbo hilo jana Ijumaa.

Ameongeza kuwa, magaidi watatu wa kujitolea muhanga wanaoaminika kuwa wanachama wa genge la kigaidi la Boko Haram ni miongoni mwa watu waliouawa katika mashambulizi hayo.

Ramani ya Nigeria inayoonyesha eneo la Maiduguri

Mwezi uliopita, watu 11 waliuawa katika makabiliano kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram katika mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Hii ni katika hali ambayo, ujumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Ijumaa ulianza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika, itakayoangazia athari za hujuma za kundi la Boko Haram.

Baraza la Usalama la UN limesema wajumbe hao wanazitembelea nchi za Nigeria, Cameroon na eneo la Ziwa Chad, kutathmini hali mbaya ya  kibinadamu inayowakabili mamilioni ya watu, kutokana na mashambulizi ya Boko Haram.

 

Tags