Apr 28, 2017 14:44 UTC
  • Ugonjwa usilojulikana waibuka Liberia, 9 wapoteza maisha

Watu tisa wamepoteza maisha na wengine wanane bado wako hospitalini nchini Liberia baada ya kuibuka ugonjwa usiojulikana na kuwakumba watu 17 tangu siku ya Jumatatu ya Aprili 24.

Shirika la Afya Duniani WHO limesema, limepokea taarifa kutoka Wizara ya Afya ya Liberia kuhusu ugonjwa huo usiojulikana na vifo kwenye hospitali ya Francis Grant mjini Greenville, kata ya Sinoe, Kusini Mashariki mwa mji mkuu Monrovia.

Idadi kubwa ya waathirika ni vijana walio chini ya umri wa miaka 21. Hata hivyo WHO imesema, vipimo vimeonyesha kuwa ugonjwa huo si wa Ebola. Fadela Chaib ni msemaji wa WHO; amesema, timu za dharura zimewekwa tayari katika ngazi ya Wilaya na Kata kwa msaada wa kiufundi na vifaa kutoka WHO na wadau wengine. Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa, kutapika, maumivu ya kichwa, na kuharisha.

Maafisa wa afya wakikabiliana na ugonjwa wa Ebola

Timu za dharura zinachunguza ripoti zinazouhusisha mripuko wa ugonjwa huo na kuhudhuria mazishi ya kiongozi mmoja wa dini.

Mwezi Juni mwaka jana, Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza rasmi kumalizika homa ya ugonjwa hatari ya Ebola baada ya miaka miatatu ya kushuhudiwa nchini humo na kusababisha idadi kubwa ya watu kupoteza maisha.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani, kuanzia mwezi Disemba mwaka 2013, hadi Juni 2016, karibu watu 26  elfu waliripotiwa kuambukizwa ugonjwa huo hatari huku wengine 11 elfu wakipoteza maisha.

Tags