May 13, 2017 07:11 UTC
  • Ugonjwa wa Ebola waripotiwa DRC, watu watatu wafariki dunia

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, ugonjwa wa Ebola umezuka katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kwamba, hadi sasa watu watatu wamefariki dunia kwa ugonjwa huo hatari.

Taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) imesema kuwa, mlipuko wa ugonjwa huo umeathiri maeneo ya msituni ya Aketi, katika mkoa wa Bas-Uele karibu na mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Shirika hilo limesema kuwa, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Oly Kalenga alisema kupitia barua, kulikuwa na watu tisa kutoka eneo la kiafya la Likati, Aketi waliohofiwa kuwa na Ebola.

Watano kati yao walipimwa na mmoja wao akathibitishwa kuwa na virusi hivyo. Watatu kati ya tisa hao walifariki. Waziri huyo alikuwa ameiandikia WHO barua akiomba usaidizi katika kudhibiti ugonjwa huo.

Ebola ilivyolikumba eneo la magharibi mwa Afrika 2014 na 2015

Mnamo mwaka 2014, mkurupuko wa ugonjwa huo Congo DR ulidhibitiwa kwa haraka ingawa watu 49 walifariki dunia.

Itakumbukwa kuwa, watu zaidi ya 11,000 walifariki dunia kutokana na mlipuko wa ugonjwa  wa Ebola katika eneo la Afrika Magharibi mwaka 2014 hadi 2015,hususan nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia katika mlipuko wa Ebola ulioatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kutokea duniani.

Ebola ni aina ya ugonjwa ambao mgonjwa hutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili na ambao huambukizwa mtu iwapo atagusana  moja kwa moja na damu au maji maji yanayotoka mwillini kwa mgonjwa.

 

Tags