Watu 33 wauawa katika mapigano ya wakulima na wafugaji nchini Nigeria
Watu 33 wameripotiwa kupoteza maisha katika mapigano makali baina ya wakulima na wafugaji, katikati mwa Nigeria.
Polisi ya Nigeria imetangaza kuwa mapigano hayo makali ya siku mbili ambayo yamewahusisha wafugaji wa kabila la Fulani na jamii za wakulima yamejiri katika kijiji cha Kajuru, kilichopo katika jimbo la Kaduna. Inaelezwa kuwa mapigano hayo yaliibuka baada ya wanakijiji kuwashambulia baba na kijana mmoja wa kabila la Fulani. Mapigano na tofauti juu ya umiliki wa ardhi kati ya wafugaji na wakulima, ni mambo ambayo yamekuwa yakitokea kila mara nchini Nigeria.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na serikali ya Abuja, maelfu ya watu wamepoteza maisha katika mapigano hayo ya kuwania ardhi ndani ya kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, hususan katika maeneo ya katikati mwa nchi. Mbali na migogoro hiyo ya ardhi, Nigeria pia inakabiliwa na mgogoro wa ndani unaosababishwa na uepo wa makundi yanayochafua usalama na amani kama vile kundi la kigaidi la Boko Haram, Niger Delta na kundi la wapiganaji wanaotaka kujitenga la Mend.