Mar 18, 2016 14:42 UTC
  • Shambulizi dhidi ya msikiti Nigeria laendelea kulaaniwa

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali shambulizi la kigaidi lililolenga msikiti nchini Nigeria na kuua watu 25.

Taarifa iliyotolewa na Ban Ki-moon imelaani vikali shambulizi hilo la kigaidi lililofanyika dhidi ya msikiti wa Waislamu katika viunga vya mji wa Maiduguri kwenye jimbo la Borno huko kaskazini mwa Nigeria na ametoa wito wa kushughulikiwa majeruhi wa shambulizi hilo. Vilevile Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo la kigaidi.

Jumanne iliyopita wanawake wawili waliokuwa wamevaa nguo za kiume walishambulia Waislamu waliokuwa katika ibada ya Swala ya Alfajiri msikitini katika eneo la Mulai mjini Maiduguri katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua Waislamu 25. Waumini wengine zaidi ya 30 walijeruhiwa. Hilo ni shambulio la pili kufanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram huko kaskazini mwa Nigeria katika mwezi huu wa Machi.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria pia alikuwa tayari ametoa ujumbe akilaani shambulizi hilo lililofanywa na magaidi wa kundi la Boko Haram na kusema shambulizi hilo dhidi ya nyumba ya ibada limeonesha tena kwamba, watekelezaji wake wanaodai kulinda dini ni watenda jinai na wahalifu wasiokuwa na nafasi yoyote katika jamii iliyostaarabika. Rais Buhari amesisitiza kuwa, vyombo vya upelelezi na usalama vimeazimia kung'oa kabisa mzizi wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria.

Tangu aliposhika hatamu za kuongoza Nigeria, Rais Muhammadu Buhari alitangaza kuwa suala la kupambana na Boko Haramu linapewa kipaumbele kikubwa katika ajenda ya kazi za serikali yake. Mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 pia Buhari alitangaza kuwa, jeshi la Nigeria limelishinda kundi hilo la kigaidi. Hata hivyo inashuhudiwa kuwa magaidi wa kundi hilo wangali wanafanya mashambulizi na mauaji ya kutisha katika maeneo mbalimbali ya Nigeria. Kwa msingi huo wachambuzi wa mambo wanasema, japokuwa kumechukuliwa hatua kadhaa katika mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram lakini hadi sasa hakuna maendeleo makubwa na ya kuridhisha katika uwanja huo.

Takwimu zinazonesha kuwa, mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram katika maeneo yenye idadi kubwa ya Waislamu huko kaskazini mwa Nigeria yameua watu karibu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi. Aghlabu ya mashambulizi ya Boko Haram yamekuwa yakilenga maeneo ya umma kama masoko, shule na kadhalika japokuwa katika siku za hivi karibuni kundi hilo limezidisha mashambulizi ya kigaidi dhidi ya misikiti.

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanalilaumu jeshi la Nigeria kuwa halichukui hatua za kutosha za kukabiliana na kundi hilo la kigaidi na wengine wanasema baadhi ya makamanda wa jeshi la Nigeria wanakwamisha mapambano ya kulitokomeza kundi hilo. Vilevile kuna wafuatiliaji wa mambo wanaosisitiza kuwa, baadhi ya nchi za kigeni zinalisaidia kwa siri kundi la kigaidi la Boko Haram.

Miezi kadhaa iliyopita jeshi la Nigeria lilishambulia shughuli za kidini za Waislamu wa mji wa Zaria na kuua mamia miongoni mwao. Jeshi hilo pia limemtia nguvuni kiongozi wa Waislamu wa mji huo Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe ambao wanaoendelea kushikiliwa hadi hivi sasa.

Wataalamu wa mambo wanasema nchi ya Saudi Arabia imezidisha harakati za kueneza itikadi na fikra za kitakfiri na kiwahabi hususan katika bara la Afrika na wanasisitiza kwamba kuna ushahidi madhubuti wa kuwepo mfungamano mkubwa baina ya makundi ya kitakfiri kama Boko Haram na stratijia ya sasa ya watawala wa kifalme wa Saudia. Vilevile hatupasi kusahau harakati za baadhi ya nchi kama Marekani na muitifaki wake mkubwa, utawala haramu wa Israel, ambao daima hupendelea kuwinda samaki katika maji machafu.

Tags