Wakenya washiriki uchaguzi wa rais wa marudio uliosusiwa na upinzani
Wananchi wa Kenya waliotimiza masharti ya kupiga kura wameelekea katika masanduku ya kupigia kura kushiriki uchaguzi wa marudio wa urais, ambao umesusiwa na viongozi na wafuasi wa upinzani.
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema alfajiri katika zoezi la kidemokrasia ambalo limeligawa taifa, baada ya kinara wa muungano wa upinzani Raila Odinga kuwataka wafuasi wake kutoshiriki.
Baadhi ya wapiga kura wameripotiwa kuanza kupiga foleni kuanzia saa kumi na moja alfajiri hususan katika ngome za chama tawala Jubilee, kama vile kaunti ya Murang'a na Uasin Gishu.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, maafisa wa polisi mjini Kisumu wamelazimika kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya vijana waliokuwa wanarusha mawe na kujaribu kuvuruga shughuli za uchaguzi.
Aidha polisi wamedhibiti hali katika mtaa wa mabanda wa Kibra jijini Nairobi, baada kundi la vijana kufunga barabara na kuchoma moto matairi.
Hapo jana, Odinga aliwatolea wito wafuasi wake kusususia uchaguzi wa marudio wa rais wa leo akisisitiza kwamba ataongoza kampeni ya uasi wa kiraia dhidi ya serikali.
Kiongozi huyo wa upinzani amekataa kushiriki katika uchaguzi huu akisema kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya nchi hiyo IEBC imeshindwa kutekeleza marekebisho ili kuzuia uchaguzi mwingine wenye kasoro.
Itakumbukwa kuwa, uchaguzi huu wa marudio wa rais unafanyika baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kutengua ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 8, kwa msingi kuwa uligubikwa na dosari.