Mar 23, 2016 07:17 UTC
  • Ebola yaua watu 5 Guinea, maambukizi 800 yanachunguzwa

Mripuko wa homa hatari ya Ebola nchini Guinea Conakry umesababisha vifo vya watu watano huku mamia ya wengine wakiaminika kuwa tayari wameambukizwa ugonjwa huo.

Wizara ya Afya ya nchi hiyo imesema kuwa, mripuko huo mpya umetokea katika kijiji cha Porokpara, kusini mashariki mwa nchi. Fode Tass Sylla, msemaji wa kitengo cha Wizara ya Afya kinachoshughulikia ugonjwa huo amesema yumkini watu 818 kutoka familia 107 wameambukizwa homa hiyo hatari katika kijiji cha Porokpara na kwamba wametuma timu ya madaktari kwenda kudhibiti hali. Amesema kuwa watu hao watawekwa karantini kwa muda wa siku 21 ili kuzuia maambukizi zaidi.

Kesi mpya mbili za Ebola zilithibitishwa Ijumaa iliyopita Kusini mwa mkoa wa Nzérékoré nchini Guinea Conakry. Kesi mpya zilithibitishwa siku ambayo Shirika la Afya Duniani WHO lilitangaza kumalizika kwa mripuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani ya Sierra Leone.

Ebola imeua zaidi ya watu 11,300 tangu mwezi Desemba 2013 katika mripuko mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa wa ugonjwa huo uliozikumba zaidi nchi tatu za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.

Tags