Magufuli na Museveni walaani uamuzi wa ICC kuhusu Burundi
Marais wa Tanzania na Uganda wamelaani uamuzi ulitolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), ambayo imemuagiza Mwendesha Mashtaka wake, Fatou Bensouda kuanzisha uchunguzi wa vitendo vya kihalifu dhidi ya binadamu vilivyotokea nchini Burundi.
Rais John Magufuli wa Tanzania amelaani uamuzi wa mahakama hiyo leo Jumamosi Novemba 11, 2017 akiwa mjini Masaka nchini Uganda kabla ya kuagana na mwenyeji wake, Rais Yoweri Museveni baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku tatu.
Rais Tanzania amesema, “Hatua hii inarudisha nyuma jitihada zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyounda kamati ya usuluhishi wa mgogoro wa Burundi inayoongozwa na Rais Museveni na Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa.”
Amesema hali ya Burundi si mbaya kama inavyotangazwa kwa kuwa tayari wakimbizi wengi waliokuwa Tanzania wamerejea nchini humo, huku wengine wakiendelea kurejea.
Rais Magufuli amesema viongozi wanaosuluhisha mgogoro huo wamepanga kukutana Novemba 23,2017 kuendeleza mchakato wa utatuzi.
Akizungumzia suala hilo, Rais Museveni wa Uganda ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amesema ICC inaingilia mambo ya jumuiya hiyo bila kuwahusisha viongozi wake jambo ambalo si sahihi na linarudisha nyuma juhudi za kutafuta amani ya Burundi.
Majaji wa ICC Juzi tarehe 9 Novemba walimtaka Mwendesha Mashtaka wa mahakama hiyo kuchunguza vitendo vya kihalifu dhidi ya binadamu vilivyotokea Burundi tangu kuzuka kwa mvutano wa ndani miaka miwili iliyopita.
Wakati huo huo vyama vya upinzani nchini Burundi vimetangaza kuunga mkono mpango huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai. Charles Nditije, kinara wa jukwaa la upinzani la CNARED ambaye yuko uhamishoni ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa: "Huu ni ushindi mkubwa kwa mfumo wa sheria nchini Burundi, na ni ushindi kwa wale wanaotaka kurejesha amani na utawala wa sheria nchini humo."
Kibali cha kufanyika uchunguzi kuhusu uhalifu ulizofanyika huko Burundi kimetolewa baada ya Mwendesha Mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda kusema kuwa, uchunguzi wake umepata ushahidi unaothibitisha kuwa polisi na askari usalama wa serikali ya Burundi walifanya mashambulizi ya makusudi dhidi ya raia. Bensouda ameongeza kuwa, mashambulizi hayo yalihusisha "vitendo vingi vya mauaji, vifungo, mateso, ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kingono, kupotezwa raia na kadhalika.
Taarifa ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai imesema kuwa, inakadiriwa kwamba watu 1200 wameuawa, maelfu wameswekwa jela kinyume cha sheria, maelfu ya wengine wameteswa na mamia wametoweka.