Answarullah ya Yemen yaiunga mkono Somalia; yaionya Imarati
Muhammad Ali al Houthi, mkuu wa Kamati Kuu za Mapinduzi ya Yemen ameiunga mkono Somalia katika mgogoro wake na Imarati ambayo inaingilia waziwazi masuala ya ndani ya Somalia na kuitahadharisha Abu Dhabi kwa kuingilia masuala ya ndani ya Mogadishu.
Imeripotiwa kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu unaingilia waziwazi masuala ya ndani ya Somalia ikiwa ni pamoja na kumuunga mkono Hasan Sheikh Mahmoud, rais wa zamani wa Somalia na hilo limewakasirisha viongozi wa hivi sasa wa nchi hiyo ambao wameishitaki Imarati kwa Umoja wa Mataifa wakiitaka iheshimu haki ya kujitawala Somalia.

Serikali ya Mogadishu pia imelishutumu shirika la bandari la Dubai kwa kuvunja waziwazi haki ya kujitawala Somalia na kuhatarisha umoja na mshikamano wa nchi hiyo.
Gazeti la al Quds al Arabi limemnukuu Muhammad Ali al Houthi, mkuu wa Kamati Kuu ya Mapinduzi ya Yemen akiandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Answarullah ya Yemen inalaani uingiliaji wa Imarati katika masuala ya ndani ya Somalia na kuitaka iache kufanya hivyo.
Uvamizi wa Saudi Arabia nchini Yemen umezusha mgogoro mkubwa katika eneo la Ghuba ya Uajemi, Afrika Kaskazini na Pembe ya Afrika huku nchi nne za Saudia, Imarati, Bahrain na Misri zikikata uhusiano wao wote na Qatar, kama ambavyo Somalia ambayo inapakana na Yemen nayo haikusalimika na athari mbaya za uvamizi huo.