Mufti Mkuu wa Libya aishambulia Imarati kwa kuchochea machafuko nchini mwake
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45910-mufti_mkuu_wa_libya_aishambulia_imarati_kwa_kuchochea_machafuko_nchini_mwake
Mufti Mkuu wa Libya, Sheikh Sadiq al Ghariani ameushambulia vikali Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwa kueneza fitna na kuchochea chuki na uhasama katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 16, 2018 04:04 UTC
  • Mufti Mkuu wa Libya aishambulia Imarati kwa kuchochea machafuko nchini mwake

Mufti Mkuu wa Libya, Sheikh Sadiq al Ghariani ameushambulia vikali Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) kwa kueneza fitna na kuchochea chuki na uhasama katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Mufti huyo wa Libya amelaani mauaji yanayofanyika katika mji wa mashariki mwa Libya wa Derna kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na kusema kuwa, madai ya kuweko magaidi katika mji wa Derna ni uongo wa wazi.

Mji wa Derna nchini Libya

 

Televisheni ya al Ebaa imemnukuu Sheik Ghariani akisema hayo jana Ijumaa na kuongeza kuwa, chuki na fitna iliyotokea Libya na katika nchi nyingine za Kiarabu katika kile kilichodaiwa kuwa ni "Arab springs" vyote vimepangwa na 'Timu ya Wazayuni' inayofanya kazi zake katika Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati). 

Matamshi hayo ya Mufti Mkuu wa Libya yamekuja baada ya kuenea mkanda wa video katika mitandao ya kijamii unaowaonesha wanajeshi wanaoungwa mkono na Imarati wa Jenerali Khalifa Haftar wakiuwa watu wawili wasiojulikana huko Derna. Ukwenzi na ukelele wa mmoja wa watu hao unasikika kwenye mkanda huo wa video muda mchache kabla ya kupigwa risasi na kuuawa. Video hiyo pia inawaonesha wanajeshi wa Khalifa Haftar wakimshambulia mwanamme mwengine mmoja baada ya kumlazimisha kuvua nguo na viatu na hapo hapo walimpiga risasi na kumuua.

Wapiganaji wa Khalifa Haftar wakiingia katika mji wa Derna, mashariki mwa Libya

 

Sehemu nyingine ya video hiyo inawaonesha wanajeshi wa Jenerali Khalifa Haftar wakiichezea na kuifanyia istihzai maiti ya Abdu Zayd al Shalawi, mmoja wa wapiganaji wa Kikosi cha Ulinzi wa Derna (DPF) aliyeuliwa vitani na wanajeshi hao wa wanaosaidiwa kikamilifu na Imarati.

Maeneo yaliyotekwa na vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar huko Derna vimekuwa vikishuhudia vitendo vya ulipizaji kisasi ikiwemo kutiwa mbaroni maimamu wa sala za jamaa na kutupwa kwenye jela za kuogofya. 

Derna ni mji wa mwisho mkubwa wa mashariki mwa Libya ambao haujatekwa na wanajeshi wa Jenerali Khalifa Haftar ingawa umezingirwa na wanajeshi hao kwa karibu miaka miwili sasa.

Athari za mapigano Derna Libya