Rais wa zamani wa Tunisia: Saudia na Imarati ni hatari kwa demokrasia
-
Moncef Marzouki
Rais wa zamani wa Tunisia ametahadharisha kuhusu njama zinazofanywa na Saudi Arabia na Imarati kwa ajili ya kuingilia uchaguzi mkuu ujao nchini humo.
Moncef Marzouki amesema kuwa, Imarati na Saudi Arabia ni hatari kubwa kwa demokrasia nchini Tunisia na zinafanya njama za kuvuruga matunda ya mapinduzi ya wananchi nchini humo.
Rais wa zamani wa Tunisia amevitahadharisha vyama na makundi ya kisiasa nchini humo na kuyataka yasikubali misaada ya kifedha kutoka Saudia na Imarati. Amesema kuwa, safari ya siku chache zilizopita ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia nchini Tunisia imefanyika kwa malengo hayo ya kufifiza mapinduzi ya watu wa Tunisia na kuvuruga matunda yake.
Moncef Marzouki amekosoa hatua ya serikali ya sasa ya Tunisia ya kumkaribisha Muhammad bin Salman nchini humo na kusema lilikua kosa la kisiasa na kimaadili na kwamba, kama angekuwepo bado madarakani asingemkaribisha Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia nchini humo.
Safari ya siku tatu ya Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudia nchini Tunisia ilikabiliwa na maandamano na upinzani mkubwa wa wananchi na taasisi mbalimbali za kiraia zinazomtambua Muhammad bin Salman kuwa ni muuaji wa watoto wa Yemen na mkandamizaji wa maulamaa na wanafikra wa Kiislamu.