Msumbiji: Raia wa Tanzania na Afrika Kusini ndio wanaoongoza 'al-Shabaab'
Waendesha Mashitaka nchini Msumbiji wamewataja raia wawili wa Tanzania na mmoja wa Afrika Kusini kuwa miongoni mwa makamanda wa kundi la kigaidi la al-Shabaab ambalo hapo awali lililikuwa linajiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, linalofanya hujuma za umwagaji damu katika mkoa wa Cabo Delgado, kaskazini mwa nchi.
Taarifa ya waendesha mashitaka hao wa Msumbji imesema Andre Mayer Hanekom raia wa Afrika Kusini na Watanzania Chafim Mussa na Adamu Nhaungwa Yangue ni miongoni mwa viongozi za ngazi za juu wa genge hilo la kigaidi waliokamatwa hivi karibuni, na wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji, jinai dhidi ya dola, kuchochea uvunjwaji wa sheria za nchi, miongoni mwa mashitaka mengine.
Hivi karibuni serikali ya Msumbiji ilisema wapiganaji wa kundi la al Shabab wameua raia zaidi 50 wa nchi hiyo, mbali na kuchoma moto vijiji kadhaa na kuwalazimisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao katika eneo hilo. Haijabainika iwapo kundi hilo la kigaidi la Msumbiji lina mfungamano wowote na kundi la kigaidi na kitakfiri al-Shabaab la Somalia au la.
Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikisumbuliwa na mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi hilo linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.
Baada ya kushadidi hujuma hizo, serikali ya Msumbiji ilituma wanajeshi na polisi katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Tanzania na tayari imewakamata mamia ya washukiwa.
Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka uliomalizika, watu 12 waliuawa katika shambulizi la kigaidi kaskazini mwa Msumbiji, ambapo vyombo vya usalama nchini humo vilidai kuwa, miongoni mwa magaidi waliohusika na jinai hiyo ni pamoja na raia wa Tanzania, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.