Somaliland yalalamikia hatua ya Somalia kumtimua mjumbe wa UN
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50621-somaliland_yalalamikia_hatua_ya_somalia_kumtimua_mjumbe_wa_un
Jamhuri iliyojitangazia uhuru ya Somaliland nchini Somalia imekosoa vikali hatua ya serikali ya Mogadishu ambayo Jumanne iliyopita ilimfukuza nchini humo Nicholas Haysom, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, kutokana na kile ilichokitaja kama mienendo yake mibaya na kuingilia kwake waziwazi mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 03, 2019 23:20 UTC
  • Somaliland yalalamikia hatua ya Somalia kumtimua mjumbe wa UN

Jamhuri iliyojitangazia uhuru ya Somaliland nchini Somalia imekosoa vikali hatua ya serikali ya Mogadishu ambayo Jumanne iliyopita ilimfukuza nchini humo Nicholas Haysom, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, kutokana na kile ilichokitaja kama mienendo yake mibaya na kuingilia kwake waziwazi mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Katika taarifa, Somaliland imesema Nicholas Haysom amefanya kazi nzuri inayopaswa kupongezwa tangu kuteuliwa kwake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres mwezi Septemba mwaka uliomalizika 2018, kuwa mjumbe maalumu wa UN katika masuala ya Somalia.

Serikali ya Somaliland imesema inaitakidi kuwa, uamuzi huo wa serikali ya Mogadishu ya kumfukuza mwakilishi wa UN umechochewa na ajenda fiche, na huenda kitendo hicho kikawa na taathira hasi kwa kanda hiyo.

Nicholas Haysom, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa aliyetimulia Somalia

Wakati huohuo, Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo unatathmini kwa kina kitendo hicho cha kutimuliwa mwanadiplomasia wake na kwamba katika wakati mwafaka utatangaza hatua utakazochukua kufuatia jambo hilo.

Itakumbukwa kuwa, Jumatatu iliyopita, Haysom aliwataka viongozi wa Somalia watoe maelezo kuhusu kutiwa mbaroni Mukhtar Robow, mmoja wa viongozi wa zamani wa genge la kigaidi la al Shabab ambaye pia aliwahi kuwa mgombea katika uchaguzi wa nchi hiyo, pamoja na wafuasi wake 15 waliowekwa nguvuni wakati wa maandamano ya tarehe 13 Disemba 2018 mjini Baidoa.