Somalia yakataa ombi la kuangalia upya uamuzi wa kumfukuza mjumbe wa UN
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya kufukuzwa nchini Somalia, Nicholas Haysom, mjumbe maalumu wa umoja huo katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, lakini amesisitiza kuwa nafasi hiyo itajazwa katika siku chache zijazo.
Akiongea na waandishi wa habari mjini New York jana Ijumaa, Naibu Msemaji wa UN Farhan Haq amesema Antonio Guterres amesikitishwa mno na kitendo hicho cha kutimuliwa mwanadiplomasia huyo nchini Somalia, lakini karibuni hivi atamteua mjumbe mwingine kwenda kujaza nafasi ya Haysom.
Amesema Guterres amezungumza mara mbili kwa njia ya simu na Rais wa Somalia, Mohammed Abdullahi Farmajo kuhusiana na kadhia hii, lakini ameshindwa kuishawishi serikali ya Mogadishu kuangalia upya uamuzi wake huo.
Hiyo jana pia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao cha faragha kutathmini uamuzi huo wa Somalia wa kumfukuza Nicholas Haysom.
Jamhuri iliyojitangazia uhuru ya Somaliland nchini Somalia imekosoa vikali hatua hiyo ya serikali ya Mogadishu ya kumfukuza nchini humo Nicholas Haysom, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa, kutokana na kile ilichokitaja kama mienendo yake mibaya na kuingilia kwake waziwazi mambo ya ndani ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Itakumbukwa kuwa, Jumatatu iliyopita, Haysom aliwataka viongozi wa Somalia watoe maelezo kuhusu kutiwa mbaroni Mukhtar Robow, mmoja wa viongozi wa zamani wa genge la kigaidi la al Shabab ambaye pia aliwahi kuwa mgombea katika uchaguzi wa nchi hiyo, pamoja na wafuasi wake 15 waliotiwa nguvuni wakati wa maandamano ya tarehe 13 Disemba 2018 mjini Baidoa.