Jeshi la Burkina Faso lathibitisha kuua magaidi 146 kusini mwa nchi
Jeshi la Burkina Faso limethibitisha kuwa limeua makumi ya wanachama wa magenge ya kigaidi katika operesheni tatu za kulipiza kisasi, kusini magharibi mwa nchi.
Jenerali Moise Minoungou, kamanda wa ngazi za juu wa jeshi hilo amesema mashambulizi ya anga na nchi kavu ya Jeshi la Burkina Faso yameua wanachama 146 wa makundi ya kitakfiri katika maeneo ya Bahn, Bomboro na Boucle du Mouhoun karibu na mpaka wa Mali.
Amesema hakuna hata askari mmoja wa nchi hiyo aliyeuawa katika operesheni hizo, ingawaje wanajeshi kadhaa wamepata majeraha madogo.
Operesheni hizo za jeshi la Burkina Faso za jana jioni zilifanyika masaa machache baada ya watu wasiopungua 14 kuuawa katika shambulizi lililofanywa na kundi la kitakfiri na kiwahabi nchini humo.
Haya yanajiri wiki moja baada ya watu wasiopungua 10 kuuawa katika shambulio la kigaidi katika Kijiji cha Sikiré, kilomita ishirini kutoka Manispaa ya Arbinda, katika mkoa wa Soum, nchini Burkina Faso.
Makundi ya wanamgambo wenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa Al-Qaeda ndiyo ambayo yamekuwa yakituhumiwa kuhusika na hujuma hizo nchini Burkina Faso.