Feb 06, 2019 15:25 UTC
  • HRW: Jeshi la Burkina Faso limewaua watuhumiwa mbele ya familia zao

Mashiriki ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yamelituhumu jeshi la serikali ya Burkina Faso kuwa limewaua kinyama watuhumiwa wa vitendo vya kigaidi tena mbele ya watu wa familia zao.

Tuhuma hizo zimetolewa baada ya Jeshi la Burkina Faso kuthibitisha kuwa limeua makumi ya wanachama wa magenge ya kigaidi katika operesheni tatu za kulipiza kisasi, huko kusini magharibi mwa nchi.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yana wasiwasi kwamba, ukatili huo yumkini ukachochea machafuko zaidi nchini Burkina Faso kama ilivyo katika nchi jirani ya Mali ambako makundi ya kigaidi yamesababisha mapigano ya kikabila.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kanda ya Sahel huko barani Afrika, Corinne Dufka amesema kuwa, baadhi ya watuhumiwa wa vitendo vya ugaidi wameuawa mbele ya familia zao na kusisitiza kuwa, pande zote zinapaswa kujiepusha kuwaadhibu watu kwa umati. Dufka amesema kuwa hivi karibuni shirika hilo litachapisha ripoti kamili kuhusu ukatili uliofanywa na magaidi na maafisa usalama wa serikali ya Burkina Faso.

Burkina Faso

Jumatatu iliyopita Jenerali Moise Minoungou, kamanda wa ngazi za juu wa jeshi hilo alisema mashambulizi ya anga na nchi kavu ya Jeshi la Burkina Faso yameua wanachama 146 wa makundi ya kitakfiri katika maeneo ya Bahn, Bomboro na Boucle du Mouhoun karibu na mpaka wa Mali.

Operesheni hizo za jeshi la Burkina Faso zilifanyika masaa machache baada ya watu wasiopungua 14 kuuawa katika shambulizi lililofanywa na kundi la kitakfiri na kiwahabi nchini humo.  

Tags