Kushinda tena Urais "Muhammadu Buhari" na kibarua kigumu anachokabiliwa nacho
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51840-kushinda_tena_urais_muhammadu_buhari_na_kibarua_kigumu_anachokabiliwa_nacho
Tume ya Uchaguzi ya Nigeria jana ilitangaza rasmi kuwa Muhammadu Buhari ameibuka mshindi baada ya kumbwaga mshindani wake mkuu Atiku Abubakar na hivyo kupata fursa ya kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili.
(last modified 2026-02-05T12:50:29+00:00 )
Feb 28, 2019 02:29 UTC
  • Kushinda tena Urais

Tume ya Uchaguzi ya Nigeria jana ilitangaza rasmi kuwa Muhammadu Buhari ameibuka mshindi baada ya kumbwaga mshindani wake mkuu Atiku Abubakar na hivyo kupata fursa ya kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili.

Uchaguzi wa Rais nchini Nigeria ulifanyika katika hali ambayo, Muhammadu Buhari alisimama kugombea kwa tiketi ya chama tawala  cha All Progressive Congress (APC) huku mpinzani wake Atiku Abubakar akiwa mgombea Urais kwa tiketi ya chama cha PDP. Kwa mujibu wa matokeo rasmi ya Tume ya Uchaguzi, Buhari amejipatia zaidi ya kura milioni 15 ambazo ni sawa na asilimiia 55 ya kura huku mpinzani wake Atiku Abubakar akipata kura milioni 11 na laki mbili ambapo ni sawa na asilimia 41.  

Wakati wa kampeni za uchaguzi wa Rais, Muhammadu Buhari aliwataka wapiga kura wampatie fursa nyingine ili aweze kukabiliana na ufisadi, ukosefu wa usalama na kuboresha hali mbaya ya uchumi wa nchi hiyo. Uchaguzi wa Rais nchini Nigeria ulifanyika katika hali ambayo, maafisa wa ngazi za juu wa Nigeria walikuwa wametahadharisha kuhusiana na uingiliaji wa aina yoyote wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo na tuhuma za kufanyika udanganyika katika uchaguzi huo wakisisitiza juu ya kufanyika uchaguzi salama na huru.

Atiku Abubakar kiongozi wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi wa Rais nchini Nigeria

Licha ya ahadi hizo, siku chache zilizopita kulishuhudiwa kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu baada ya uchaguzi huo. Chama cha upinzani cha Atiku Abubakar kinaituhumu serikali kwamba, imefanya udanganyifu na kuiba kura. Hata hivyo chama tawala cha APC kimepinga vikali tuhuma hizo na kumtaka Atiku Abubakar akubali matokeo na kushindwa kwake katika uchaguzi huo.

Hamid Ali, wakala wa chama tawala katika hafla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi amewaambia waandishi wa  kwamba: Daima kila mtu anayeshindwa katika uchaguzi huanza kulalamika.

Mvutano wa uchaguzi unaendelea nchini Nigeria katika hali ambayo, Rais Muhammadu Buhari anakabiliwa na kibarua kigumu katika muhula wa piili wa uongozi wake. Buhari anatarajiwa kuanza muhula wa pili wa uongozi wake katika hali ambayo, anakabiliwa na kibarua kigumu katika miaka minne ijayo kwani licha ya ahadi alizotoa awali ameshindwa kuboresha hali ya uchumi na usalama katika muhula wa kwanza wa uongozi wake. Kiasi kwamba, wananchi wa Nigeria hawaridhishwi na utendaji wake hasa katika uga wa usalama na uchumi.

Mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram hadi sasa yameuawa na kujeruhi maelfu ya  watu nchini Nigeria na hali hii ya ukosefu wa usalama ingali inaendelea katika nchi hiyo. Zimwi la ufisadi, matatizo ya kiuchumi, umasikini na ukosefu wa ajira nayo ni matatizo mengine yanayoikabili nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Licha ya kuwa kabla ya kuingia madarakani, Rais Buhari aliahidi kupambana na ufisadi, lakini katika kipindi cha miaka minne ya muhula wa kwanza wa uongozi wake, hajapata mafanikio ya kuridhisha katika uwanja huo. Matatizo ya kiuchumi nayo yameshadidi nchini Nigeria kufuatia kuporomoka kwa bei ya nishati ya mafuta katika soko la dunia.

Hali hiyo imepelekea kuongezeka ukosefu wa ajira, umasikini na vita vya ndani vya kupigania vyanzo vya maji, ardhi na mifugo. Kwa mujibu wa ripoti za kiuchumi, wananchi milioni 87 wa Nigeria wanaishi chini ya mstari wa umasikini huku watoto milioni 13 wa nchi hiyo wakishindwa kwenda shule. 

Gazeti la Le Figaro liliandika katika toleo lake la tarehe 19 mwezi huu wa Februari kwamba: Rais ajaye wa Nigeria atakabiliwa na changamoto nyingi likiwemo suala la kuwa tegemezi kwa nishati ya mafuta, umasikini, ukosefu wa ajira na kadhalika.

Filihali inaonekana kuwa, Rais Buhari atakabiliwa na kibarua kigumu zaidi katika muhula wa pili wa uongozi katika njia ya kutekeleza ahadi zake alizoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi hususan suala la kuboresha hali ya uchumi na usalama nchini Nigeria.