Mamia ya watu watiwa nguvuni Nigeria kwa uhalifu unaohusiana na uchaguzi
Polisi ya Nigeria imetangaza kuwa, imewatia nguvuni zaidi ya watu 300 kwa tuhuma za kufanya uhalifu unaohusiana na uchaguzi wa mkuu uliofanyika mwezi uliopita.
Mkuu wa Jeshi la Polisi la Nigeria, Abubakar Mohammed Adamu amesema kuwa, watu hao wamekamatwa kwa tuhuma zinazohusiana na uhalifu na uvunjaji wa sheria za uchaguzi wa Rais na Bunge uliofanyika tarehe 23 Februari nchini humo.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi la Nigeria imesema kuwa, polisi wawili pia wameuawa katika ghasia za mtaani na wengine kadhaa wamejeruhiwa.
Takwimu za taasisi za kiraia nchini Nigeria zinaonesha kuwa, watu wasiopungua 53 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika uchaguzi wa mwezi uliopita nchini Nigeria.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari Tume ya Uchaguzi ya Nigeria alitangaza kuwa Muhammadu Buhari ameshinda kiti cha urais kwa muhula wa pili. Buhari ametangazwa mshindi licha ya uchaguzi huo kughubikwa na uakhirishaji, ghasia na matatizo ya kilojistiki.
Buhari aliyeshinda uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 56 ya kura, anakabiliwa na kibarua kigumu ikiwa ni pamoja na kufufua uchumi wa Nigeria na kupambana na wanamgambo wa Boko Haram ambao hadi sasa wameuawa maelfu ya watu kaskazini mashariki mwa nchi, wengi wao wakiwa raia wa kawaida.