Walibya waandamana kulaani hatua ya Trump kumpigia simu Jenerali Haftar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52975-walibya_waandamana_kulaani_hatua_ya_trump_kumpigia_simu_jenerali_haftar
Wananchi wa Libya wamefanya maandamano mjini Tripoli kukosoa hatua ya Rais Donald Trump kumpigia simu jenerali muasi Khalifa Haftar mwenye makao yake katika mji wa Benghazi, magharibi mwa Libya, na ambaye amekuwa akiendesha kampeni ya kijeshi ya kutaka kuuteka mji mkuu Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2019 08:37 UTC
  • Walibya waandamana kulaani hatua ya Trump kumpigia simu Jenerali Haftar

Wananchi wa Libya wamefanya maandamano mjini Tripoli kukosoa hatua ya Rais Donald Trump kumpigia simu jenerali muasi Khalifa Haftar mwenye makao yake katika mji wa Benghazi, magharibi mwa Libya, na ambaye amekuwa akiendesha kampeni ya kijeshi ya kutaka kuuteka mji mkuu Tripoli.

Duru za habari zinaarifu kuwa, watu zaidi ya elfu mbili walifanya maandamano katika Medani ya Mashahidi mjini Tripoli jana Ijumaa, kulaani uingiliaji huo wa Marekani katika mambo ya ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Taarifa ya Ikulu ya White House imesema kuwa, Trump anatambua eti jitihada za Khalifa Haftar katika kupambana na ugaidi na kuvilinda visima vya mafuta ya nchi hiyo.

Mbali na Marekani na Ufaransa, Jenerali Haftar anapata uungaji mkono wa hali na mali kutoka kwa tawala za Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia.

Mapigano ya kuudhibiti mji wa Tripoli

Shirika la Afya Duniani linasema kwa uchache watu 205 wamepoteza maisha tokea Aprili 4 wakati Haftar alipoanzisha oparesheni yake ya kutaka kuuteka mji wa Tripoli.

Wakati huo huo Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya imetoa waranti wa kukamatwa Haftar na maafisa wake sita kwa kuhusika katika hujuma dhidi ya maeneo ya raia.