Somalia yasambaratisha mtandao wa majasusi wa UAE
Wakuu wa Somalia wametangaza kuusambaratisha mtandao wa majasusi ambao walikuwa wakiutumikia utawala wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Gaza la al-Raya la Qatar limenukulu duru za idara ya usalama wa taifa Somalia ikisema majasusi hao wa UAE wamekamatwa katiak oparesheni maalumu.
Uhusiano baina ya Somalia na UAE ulivurugika tokea mwezi Juni 2017 wakati wakuu wa Mogadishu walipokataa mashinikizo ya Saudia na UAE na kukataa kukata uhusiano na Qatar kufuatia mgogoro baina ya nchi hizo jirani za Ghuba ya Uajemi. Somalia imesisitiza kuwa haipendelei upande wowote katika mgogoro huo wa kidiplomasia unaoendelea kutokota katika Ghuba ya Uajemi.
Aprili 9, 2018 maafisa wa usalama wa Somalia walinasa dola milioni 9.6 kutoka ndege binafsi ya UAE ambayo ilikuwa ilitua Mogadishu ikitokea Abu Dhabi. Wakuu wa Somalia walisema lengo la fedha hizo ni kuchochea fitina za kisiasa nchini humo.

Somalia pia imepinga mapatano baina ya UAE na eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland kuhusu kutumia bandari ya Berbera katika eneo hilo. Somalia imesema mapatano hayo hayana msingi wa kisheria na imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kucuhukua hatua kukabiliana na kitendo hicho.
Itakumbukwa kuwa, tarehe tano Juni 2017, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain na Misri zilikata uhusiano wao wote na Qatar na kuiwekea vikwazo vya kila upande kwa kuifungia njia zote za ardhini, angani na majini. Muungano huo wa Saudi umekiwa ukizishinikiza bila mafanikio nchi zingine kukata uhusiano na Qatar.