Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiri, ukoloni umekufa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58058-rais_wa_ufaransa_emmanuel_macron_akiri_ukoloni_umekufa
Mienendo ya nchi za Magharibi kuhusiana na bara la Afrika daima uimekuwa ya kikoloni na kuwanyonya watu wa bara hilo na wakati huo huo kukandamiza harakati za wapigania uhuru.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2019 09:17 UTC
  • Macron na Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara
    Macron na Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara

Mienendo ya nchi za Magharibi kuhusiana na bara la Afrika daima uimekuwa ya kikoloni na kuwanyonya watu wa bara hilo na wakati huo huo kukandamiza harakati za wapigania uhuru.

Hata hivyo kuporomoka nguvu za madola ya kikoloni kama Ufaransa na Uingereza na kubadilika msingi wa mahusiano na mazingira ya nchi nyingi za Afrika kumemlazimisha Rais wa Ufaransa akiri kwamba, kulifanyika makosa katika mienedo ya huko nyuma ya nchi za Magharibi kuhusiana na Afrika.

Emmanuel Macron amesema katika matamshi yake ya hivi karibuni kwamba ukoloni umekufa. Akiwa safarini katika koloni la zamani la Ufaransa yaani Ivory Coast, Macron amesema ukoloni ulikuwa kosa kubwa na ametoa wito wa kubadilishwa ukurasa wa historia. Macron amesema mjini Abidjan kwamba: "Watu wanaitazama Ufaransa kama nchi iliyokuwa na mitazamo ya kikoloni na iliyofanya ukoloni ambao ulikuwa kosa kubwa na ukiukaki wa jamhuri." Wakati wa kampeni zake za uchaguzi wa rais pia Macron alisisitiza kwamba ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria ulikuwa jinai dhidi ya binadamu, suala ambalo lilizusha ukosoaji mkubwa wa Wafaransa dhidi ya kiongozi huyo. 

Emmanuel Macron

Matamshi hayo ya aina yake ya Emmanuel Macron kama rais wa dola la kikoloni na lenye historia ya karne kadhaa za kuvamia, kuua watu na kukoloni mataifa na nchi nyingine za mashariki mwa Asia na Afrika, yanaonesha kuwa, kipindi cha ukoloni kimefikia ukingoni na madola ya kikoloni yametambua kuwa, hayawezi tena kuendeleza mahusiano yao ya kipindi cha ukoloni na nchi za Afrika zilizokuwa makoloni yao. Huwenda ni kwa sababu hiyo ndiyo maana nchi kama Ufaransa na Uingereza zinafanya jitihada za kulinda maslahi yao katika nchi za Afrika kwa kutumia mbinu nyingine kama za kuimarisha ushawishi wao barani humo na kuendelea kuzinyonya nchi hizo kwa kutumia njia mpya. 

Nukta nyingine ni kuwa Macron amefanya jitihada za kukana mfungamano wake na kipindi cha ukoloni kwa kusema kuwa, yeye si katika kizazi cha kipindi cha ukoloni. Hata hivyo ukweli ni kwamba, wazungu wa Ulaya wakiwemo Wafaransa, wangali wanalitazama bara la Afrika kwa jicho lile lile la kipindi cha ukoloni. Akihutubia raia wa Ivory Coast, Macron amewataka vijana wa nchi hiyo waanzishe kipindi kipya cha ushirikiano na Ufaransa. Maana ya "kuanzisha kipindi kipya cha kushirikiana na Ufaransa" katika matamshi haya ni kukubali ushawishi na satua ya Paris barani Afrika ikiwemo Ivory Coast. Kwa sasa Ufaransa imetuma jeshi kubwa katika nchi kadhaa makoloni yake ya zamani huko magharibi mwa Afrika kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na inajihusisha na masuala ya kisiasa ya nchi kama Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mali na Ivory Coast kwa ajili yakulinda maslahi yake katika nchi hizo.

Japokuwa nchi nyingi za Afrika zilipata uhuru na kuanza kujitawala baada ya Vita vya Pili vya Dunia, lakini Wamagharibi waliendelea kuwa na satua na ushawishi katika muundo wa siasa, uchumi na hata masuala ya kijeshi ya nchi hizo kupitia njia mbalimbali na wanafanya kila wawezalo kudumisha ushawishi huo lakini kwa sura mpya. Kuhusiana na suala hilo Rais Vladimir Putin wa Russia anasema: "Kwa sasa tunashuhudia baadhi ya nchi za Magharibi zikiamiliana na serikali za nchi za Afrika kwa kutumia mashinikizo, vitisho na kadhalika. Nchi hizo za Magharibi zinataka kudumisha ushawishi na udhibiti wao katika makoloni yao ya zamani lakini kwa mbinu na sura mpya."

Vladimir Putin

Alaa kulli hal, katika miaka ya hivi karibuni na kufuatia mabadiliko yaliyojitokeza katika muundo wa uchumi wa dunia na kudhihiri nguvu mpya za kiuchumi, ushawishi na satua ya nchi za Magharibi umepungua sana katika masoko ya biashara ya nchi za Afrika, na nchi zinazoinukia kwa kasi kiuchumi kama China, Brazil na Russia zimekuwa washirika wakubwa wa barala Afrika. Vilevile kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na madini ya aina mbalimbali, Afrika umekuwa medani ya ushindani na mpambano mkubwa baina ya wakoloni wa zamani wa bara hilo na nchi zinaoinukia kwa kasi kiuchumi.