UN: Mazungumzo ya amani Somalia ni ishara nzuri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58414-un_mazungumzo_ya_amani_somalia_ni_ishara_nzuri
Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ambaye pia ni mkuu wa mpango wa umoja huo nchini humo UNSOM jana aliliutembelea mji wa Hargesa, makao makuu ya eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland nchini Somalia na kukutana na viongozi wa eneo hilo kujadili uchaguzi na maendeleo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2020 21:05 UTC
  • UN: Mazungumzo ya amani Somalia ni ishara nzuri

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ambaye pia ni mkuu wa mpango wa umoja huo nchini humo UNSOM jana aliliutembelea mji wa Hargesa, makao makuu ya eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland nchini Somalia na kukutana na viongozi wa eneo hilo kujadili uchaguzi na maendeleo.

James Swan ambaye ametembelea eneo hilo baada ya kuwa huko mara ya mwisho miezi sita iliyopita amekutana na rais wa serikali ya eneo hilo, Musa Bihi Abdi na timu yake wakiwemo mawaziri, wawakilishi wa asasi za kiraia, viongozi wa vyama vya siasa na washirika wa kimataifa wanaofanyakazi Somaliland.

Katika majadiliano yao Swan ameishukuru serikali ya Somaliland kwa miradi ambayo amesema inalenga kujenga kujiamini na kutia nguvu majadiliano baina ya utawala wa ndani wa Hargesa na serikali kuu ya Moghadishu. 

Hargeisa makao makuu ya Somaliland

 

Mwakilishi huyo ambaye pia alikagua miradi mbalimbali ukiwemo wa ujuzi kwa ajili ya watu wenye ulemavu na wa uokozi wa wanyamapori amesema “Tumetiwa moyo na hatua zilizopigwa katika mchakato wa kukamilisha hatua zote muhimu za kufanyika uchaguzi wa Bunge hapa Somaliland 2020. 

Vile vile amemuahidi Rais na watu wa Somaliland kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kushirikiana nao kupitia miradi na ratiba mbalimbali za Umoja wa Mataifa na mashirika yake. Kwa mujibu wa mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, hivi sasa kuna mashirika 16 ya umoja huo yanatoa misaada Somaliland.