Umoja wa Mataifa wawataka viongozi wa Somalia washirikiane
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Somalia ametoa mwito kwa viongozi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kufanya kazi bega kwa bega na kuwa na ushirikiano wa karibu kwa lengo la kuhakikisha kuwa amani na uthabiti vinarejea nchini humo.
James Swan amesema kushtadi mikwaruzano ya kisiasa hakuna matokeo mengine ghairi ya kushadidisha harakati za makundi ya kigaidi na yenye misimamo ya kufurutu ada zinazotishia usalama wa nchi hiyo.
Amewataka viongozi wa Somalia kuutumia mwaka huu 2020 kutatua hitilafu na tofauti zao za kisiasa na kimitazamo ili kuhakisha kuwa maazimio yaliyofikiwa baina yao na jamii ya kimataifa mwezi Oktoba mwaka jana yanatekelezwa.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Somalia amefafanua kuwa, "Somalia haipaswi kufeli kutekeleza vipaumbele vilivyoanishwa Oktoba iliyopita kama kupunguza mzigo wa madeni, kuandaa uchaguzi, kutamatisha mchakato wa kuundwa katiba mpya, kuzipa nguvu serikali za majimbo na kupambana na kundi la kigaidi la al-Shabaab."
Amesisitiza kuwa, ili kufikia malengo haya yote, viongozi wa Somalia wanapaswa kushirikiana na kuwa na sauti moja, na kwamba jamii ya kimataifa haiwezi kupatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili nchi hiyo bila ushirikiano wa viongozi.
Kundi la kigaidi la al-Shabaab lilianzisha hujuma zake nchini Somalia mwaka 2007 na limekuwa likiendesha harakati za kigaidi katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine ya nchi hiyo.