Tunisia yapinga njama za kuigawa vipande vipande Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i60717-tunisia_yapinga_njama_za_kuigawa_vipande_vipande_libya
Rais wa Tunisia kwa mara nyingine tena ametangaza kuwa nchi yake itaendelea kupinga njama zozote za kujaribu kuigawa vipande vipande nchi jirani ya Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 01, 2020 13:45 UTC
  • Tunisia yapinga njama za kuigawa vipande vipande Libya

Rais wa Tunisia kwa mara nyingine tena ametangaza kuwa nchi yake itaendelea kupinga njama zozote za kujaribu kuigawa vipande vipande nchi jirani ya Libya.

Rais Kais Saied wa Tunisia ametoa taarifa rasmi baada ya kikao kilichojadili matukio ya hivi karibuni ya nchini Libya kilichohudhuriwa na Waziri Mkuu na mawaziri mbalimbali wa serikali yake pamoja na maafisa usalama na kijeshi kutoka Ikulu. Kikao hicho cha watu muhimu zaidi nchini Tunisia kimesisitiza kuwa Tunis inaheshimu sheria za kimataifa kuhusiana na Libya na kwamba mgogoro wa nchi hiyo inabidi utatuliwe bila ya uingiliaji wa madola ya kigeni.

Rais Kais Saied amegusia pia matatizo inayokumbana nayo Tunisia kutokana na mgogoro wa Libya na ameitaka jamii ya kimataifa kulipa umuhimu mkubwa zaidi suala la Libya.

Rais Kais Saied wa Tunisia

 

Rais huyo wa Tunisia ametoa pendekezo la kuundwa timu maalumu ya kukabiliana na matokeo mabaya yanayosababishwa na mgogoro wa Libya.

Jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya anatawala mashariki mwa Libya na tangu mwezi Aprili 2019 alianzisha vita vikubwa dhidi ya mji mkuu Tripoli kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Misri na baadhi ya nchi za Magharibi. Lengo la kuanzisha vita hilo lilikuwa ni kuiteka Tripoli na kuivunja Serikali ya Mwafaka wa Kimataifa inayotambuliwa kimataifa.

Hata hivyo ndoto za jenerali huyo muasi zimeshindwa kutimia kutokana na muqawama wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al Sarraj. 

Jumatatu wiki hii, Jenerali Khalifa Haftar alitangaza kuvunja makubaliano ya mwaka 2015 yaliyounda Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa hatua ambayo imelaaniwa kote duniani.