IOM: Wahajiri 2,300 wanazuiliwa katika mazingira ya kuogofya Libya
Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limesema maelfu ya wahajiri wanazuiliwa katika mazingira ya kutisha huko nchini Libya.
Shirika hilo limesema hayo katika ujumbe wake lilioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, "zaidi ya wahamiaji 2,300 wanazuiliwa katika mazingira ya kuogofya nchini Libya. IOM inashirikiana na mashirika ya kibinadamu kuwapa misaada ya dharura wahajiri hao, huku tukitoa mwito wa kuachiwa huru wahajiri wazee."
Kwa mujibu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa, tokea mwanzoni mwa huu hadi sasa, wahajiri zaidi ya 5,800 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameokolewa wakiwa katika safari hatarishi za baharini wakijaribu kwenda Ulaya, na kisha wakarejeshwa nchini Libya.
IOM ilikuwa imeanzisha mpango wa kuwarejesha katika nchi zao wahajiri haramu waliokwama nchini Libya, lakini ukasitishwa baada ya serikali ya Tripoli kufunga mipaka ya nchi, kama moja ya hatua za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.
Hivi karibuni, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) nchini Libya ilitoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa mauaji ya makumi ya wahajiri katika mji wa jangwani wa Mizda, yapata kilomita 160 kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri waharamu kutoka nchi mbali mbali hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.