Mamluki 160 wakamatwa Sudan wakielekea Libya kupigana vita
Sudan imesema, imewatia nguvuni watu 160 wakiwemo raia wa kigeni ambao walikuwa mbioni kuelekea Libya kwa lengo la kupigana kama mamluki katika vita vya ndani vya nchi hiyo.
Maafisa wa serikali ya Khartoum wametangaza kuwa, watu hao waliokuwa wamejigawa katika makundi mawili ya watu 80 walikuwa wakitafuta njia ili kuweza kufika nchini Libya.
Kwa mujibu wa ripoti rasmi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Imarati unakodi mamluki kutoka nchi za Afrika na kuwapeleka Libya ili wakalisaidie katika vita vya nchi hiyo kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar.
Siku ya Jumanne, mamia ya Wasudan waliandamana hadi mbele ya ubalozi wa Imarati mjini Khartoum kulalamikia kitendo cha serikali ya nchi hiyo cha kuwahadaa na kutaka kuwasafirisha na kuwapeleka vitani nchini Libya badala ya kuwapeleka Imarati kwa ajili ya kazi.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya, hivi karibuni ilitoa taarifa kulaani hatua ya Imarati ya kusajili mamluki nchini Sudan kwa ajili ya kuwapeleka vitani nchini Libya.
Imarati ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa kundi la Haftar linalojiita Jeshi la Taifa la Libya.
Kundi hilo ambalo kwa miaka kadhaa na kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi limekuwa likidhibiti eneo la mashariki ya Libya, Aprili 2019 lilianzisha hujuma na mashambulio makali dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Hatua hiyo ya kundi la Khalifa Haftar imelaaniwa na jamii ya kimataifa.
Tangu yalipofanyika mapinduzi ya wananchi mwaka 2011, yaliyopelekea kuangushwa utawala wa Muammar Gadafi, uingiliaji wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya na eneo katika vuguvugu la mapinduzi hayo umeitumbukiza Libya kwenye lindi la mapigano na machafuko ya kisiasa ambayo yangali yanaendelea hadi sasa.../