Tanzania yazuia safari za Kenya Airways nchini humo
Tanzania imesimamisha shirika la ndege la Kenya (KQ) kufanya safari za kwenda Tanzania kuanzia leo tarehe Mosi Agosti, siku moja baada ya Kenya kutangaza kuwa itafungua anga zake kwa usafiri wa kimataifa isipokuwa kutoka baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania.
Katika barua iliyotumwa kwa KQ Ijumaa ya jana Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Safari za Anga Tanzania (TCAA), Hamza S. Johari, alisema serikali ya Tanzania imesimamisha safari za KQ kati ya Nairobi na viwanja vya Tanzania kama Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar mpaka itakapotangazwa tena kujibu hatua iliyochukuliwa na serikali ya Kenya.
Jana Ijumaa serikali ya Kenya ilitangaza kufungua anga zake kwa safari za ndege za kimataifa baina ya Kenya na nchi mbalimbali zikiwemo nchi jirani za Ethiopia, Uganda na Rwanda isipokuwa Tanzania.
Tanzania na Kenya zimekuwa katika mvutano tangu kuanza kwa janga la virusi vya corona ambapo mwezi Mei nchi hizo zilifungiana mipaka kwa muda mfupi kwa madai ya kuambukizana virusi vya corona. Hatua hiyo ilitatiza usafiri wa mizigo baina ya nchi hizo kwa wiki kadha mpaka zilipokubaliana kuhusu utaratibu wa kupima madereva wa malori ya mizigo.
Tangu mwezi Aprili Tanzania haijatoa idadi ya maambuziki ya Covid-19 nchini humo na Rais John Magufuli amekaririwa mara kadha kwamba hakuna tena corona nchini humo.
Kwa upande wake Kenya imekuwa ikipambana na maambukizi ya Covid-19 na hata kufunga shughuli katika baadhi ya miji mikubwa ya nchi hiyo. Wiki hii Kenya ilitangaza hatua nyingine kadha katika jitihada za kupunguza maambuziki na hadi Ijumaa ilikuwa imetangaza maambukizi zaidi ya 20,000.