UN yawatuza mamia ya askari wa Uganda walioko Somalia
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewapa medali ya heshima wanajeshi 600 wa Uganda wanaolinda taasisi na wafanyakazi wa UN nchini Somalia.
Luteni Kanali Deo Akiiki, Naibu Msemaji wa Jeshi la Uganda amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: Askari hao wanaohudumu katika Kitengo cha Sita cha Gadi ya Umoja wa Mataifa wametuzwa medali hizo za heshima kutokana na kujitolea kwao kulinda taasisi na maafisa wa UN dhidi ya wanamgambo wa al-Shabaab.
Amesema tuzo hizo zimezotolewa na ofisi ya Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN kwa lengo la kutambua huduma za wanajeshi hao wa Uganda za kuhatarisha maisha yao katika muda wa mwaka mmoja uliopita.
Hafla ya kuwatunuku medali hizo wanajeshi hao wa Uganda nchini Somalia imeongozwa na James Swan, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Somalia, Antonio Guterres.
Mbali na kutoa huduma za ulinzi kwa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Uganda ina askari elfu sita katika Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM).