'Serikali ya Haftar' huko Libya yajiuzulu kufuatia maandamano ya wananchi
Serikali ya Libya yenye makao makuu yake mashariki mwa nchi na inayoongozwa na Abdullah Al-Thani, imetangaza kujiuzulu kufuatia maandamano ya siku tatu ya wananchi katika miji mikubwa ya mashariki mwa nchi.
Al-Thani alikabidhi barua ya kujiuzulu serikali yake kwa Spika wa Bunge la Wawakilishi wa eneo hilo, Aguila Saleh katika mkutano wa dharura uliofanyika jana Jumapili.
Wananchi wa maneo ya mashariki mwa Libya siku ya Jumamosi walichoma moto jengo la makao makuu ya serikali hiyo katika jiji la Benghazi, huku maandamano kama hayo yakishuhudiwa pia katika miji ya Al-Bayda, Sabha na Al-Marj, ngome za jenerali muasi Khalifa Haftar, anayeongoza kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) la mashariki mwa nchi.
Wananchi hao wamekuwa wakiandamana kushinikiza serikali ya eneo hilo ijiuzulu, wakisisitiza kuwa imeshindwa kuwapa huduma za msingi hususan za afya na umeme, huku kukiwa pia na ukosefu wa fedha katika benki za eneo hilo.
Wanamgambo wanaoongozwa na Khalifa Haftar ambao kwa miaka mingi sasa wanayashikilia maeneo ya mashariki mwa Libya kutokana na uungaji mkono wa hali na mali wanaopatiwa na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi walianzisha mashambulizi ya kuudhibiti mji mkuu Tripoli tangu Aprili mwaka jana; lakini hadi sasa wameshindwa kufikia lengo lao hilo.
Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa kwa upande wao zinaiunga mkono serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj, ambayo makao makuu yake yako katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.