Pakistan yaiambia UAE: Katu hatutaitambua Israel
Kwa mara nyingine tena, serikali ya Pakistan imesisitiza kuwa, kamwe haitoutambua utawala wa Kizayuni wa Israel licha ya mashinikizo ya nchi ajinabi.
Akiongea na waandishi wa habari jana Jumatatu katika mji wa Multan, Shah Mahmood Qureshi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameuhutubu Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kuuambia: Tumeweka wazi na tumeiambia bayana Imarati kuwa, kamwe Islamabad haitoitambua Israel hadi pale mgogoro wa Palestina utakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Amesema Pakistan haitakubali mashinikizo ya nchi yoyote ya kuitaka iutambue utawala ghasibu wa Israel unaokanyaga haki za wananchi wa Palestina kila leo.
Waziri wa Mashauri wa Kigeni wa Pakistan ameeleza bayana kuwa, msimamo wa taifa la Pakistan la kuwaunga mkono Wapalestina uko wazi na madhubuti.
Hivi karibuni pia, Waziri Mkuu wa Pakistan, Imran Khan alikanusha kuwepo mashinikizo ya aina yoyote ya kuitaka nchi hiyo ijiunge na safu ya nchi zinazofanya mapatano na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Alisema wananchi wa Pakistan wako bega kwa bega na wananchi wa Palestina na wanawaunga mkono kikamilifu katika kuhakikisha wanarejeshewa haki zao.