Mwakilishi wa UN Somalia alaani vikali shambulio la kigaidi la mjini Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i66372-mwakilishi_wa_un_somalia_alaani_vikali_shambulio_la_kigaidi_la_mjini_mogadishu
Umoja wa Mataifa nchini Somalia umelaani vikali shambulizi la kigaidi lilofanywa Jumapili kwenye hotel ya Afrika katika mji mkuu Mogadishu na kusababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kusalia majeruhi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 02, 2021 04:01 UTC
  • Mwakilishi wa UN Somalia alaani vikali shambulio la kigaidi la mjini Mogadishu

Umoja wa Mataifa nchini Somalia umelaani vikali shambulizi la kigaidi lilofanywa Jumapili kwenye hotel ya Afrika katika mji mkuu Mogadishu na kusababisha vifo vya watu kadhaa na wengine wengi kusalia majeruhi.

Taarifa iliyotolewa jana mjini Mogadishu, Somalia na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo James Swan imemnukuu akisema kuwa wamechukizwa na shambulio hilo kwenye eneo hilo ambalo mara nyingi hutembelewa na raia.

Kwa mujibu wa ripoti, kundi la kigaidi na ukufurishaji la Al Shabaab limekiri kuhusika na shambulio hilo la Jumapili mchana na kisha kushikilia kwa muda mrefu hoteli hiyo kabla ya kuzidiwa nguvu baadaye na vikosi vya usalama vya Somalia.

Eneo la tukio la shambulio la kigaidi mjini Mogadishu

Vyombo vya habari vinaripoti kuwa raia kadhaa waliokuwa wamekwama ndani ya hoteli waliokolewa na vikosi hivyo vya usalama vya Somalia. Bwana Swan ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wafiwa huku akiwatakia afueni ya haraka majeruhi.

Somalia iliyoko kwenye Pembe ya Afrika, imekuwa ikikabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara ya kigaidi ambapo kundi la Al Shabaab limekuwa likikiri kuhusika nayo. Katika shambulio kama hilo mwezi Agosti mwaka jana wa 2020, takribani watu 17 waliuawa baada ya magaidi hayo kushambulio hoteli ya Elite, tukio ambalo lilisababisha mapigano ya saa saba kati ya Al Shabaab na vikosi vya usalama vya Somalia.../